Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye kikao cha baraza la biashara kilichowakutanisha watumishi wa umma na sekta binafsi
Watumishi wa umma na sekta binafsi wakiwa kwenye kikao cha baraza la biashara kilichofanyika Jijini Mwanza
****************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jumla ya watoto 846,733 chini ya miaka mitano mkoania Mwanza wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya polio kuanzia April 28 hadi Mei mosi mwaka huu.
Hayo yamebainishwa Aprili 15 mwaka huu na Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja wakati wa kikao cha baraza la biashara kilichowakutanisha watumishi wa umma na sekta binafsi kilichofanyika jijini Mwanza.
Amesema kampeni ya chanjo ya polio itafanyika kwenye vituo vya kudumu na vya muda mrefu vilivyopo katika maeneo mbalimbali ikiwamo,sokoni, vituo vya mabasi, shuleni,kwenye nyumba za ibaada, mashambani, na hata kwenye makambi ya wavuvi.
Kiteleja amesema zoezi hilo litafanyika kwenye wilaya zote mkoani hapa ambapo Ukerewe chanjo inatarajiwa kutolewa kwa watoto 108,937, Magu watoto 93,721,Nyamagana watoto 92,698.
Aidha ameongeza kuwa, wilayani Kwimba takribani watoto wanaotarajiwa kupatiwa chanjo hiyo ni 134,636 Sengerema watoto 108,597 ,Ilemala watoto 85,834 na Misungwi watoto 116,167 pamoja na Buchosa watoto 106,143.
“Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano watachanjwa bila kujali kama alishapata chanjo huko nyuma hata kama alichanjwa jana, atachanjwa tena kwani chanjo hii ni salama haina madhara yoyote na baada ya kupewa chanjo hiyo mtoto atawekewa alama kwenye kidole kidogo cha mkono.
Amesema awamu ya kwanza ya zoezi hilo ilifanyika machi 24 hadi 27 mwaka 2022 katika mikoa ya Ruvuma, Songwe, Mbeya, Njombe na awamu ya pili hadi ya nne itafanyika April, Mei na Juni mwaka huu kwenye mikoa yote ya Tanzania bara
Amesema ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yoyote mwenye umri wowote ila watoto huathirika zaidi kwani unaenezwa kwa njia ya kula chakula, maji yaliyochafuliwa na vinyesi vya mtu mwenye virusi vya ugonjwa huo.
Amesema ugonjwa wa polio hauna tiba ila hukingwa kwa chanjo ya polio ambayo ipo kwa njia ya matone na sindano.
“Chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtoto anapozaliwa kabla ya siku 14,wiki 6,10 na 14 kwani anapofikia wiki 14 hupewa chanjo ya polio ya sindano (IPV)”,amesema Kiteleja.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto wa kupatiwa chanjo ya polio ili kuwakinga na ugonjwa huo.