Featured Kitaifa

MTATURU APAZA SAUTI KWENYE MAMBO SITA IKUNGI

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali kutupia jicho mambo sita katika sekta ya elimu,afya na miundombinu ya barabara ikiwemo ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika Kata ya Misughaa,Mang’onyi na Issuna.

Akichangia mjadala wa mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),April 14,2022,Mtaturu amesema anaishukuru serikali kwa kupeleka kiasi cha Shilingi Milioni 500 ambazo zimetumika katika ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Ntuntu ambapo kukamilika kwake kutaondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu.

“Katika kata 13 zilizopo katika jimbo letu,tumepata kituo hicho kimoja,hivyo niombe kupitia bajeti hii tukipata vituo hivyo vingine vitatu tutakuwa tumegusa maisha ya wananchi wa Misughaa,Mang’onyi na Issuna,”amesema.

Amesema katika ujenzi wa hospitali ya wilaya wamepata Milioni 800 ambayo inaenda kukamilisha ujenzi huo ambao unapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa watumishi wa afya ili wananchi waweze kupata huduma.

Katika sekta hiyo ya afya ameiomba serikali kupeleka waganga wakuu na manesi ili wasaidie kutoa huduma kwa wananchi.

“Kwenye sekta hii tuna upungufu mkubwa wa watumishi,kuna Zahanati unakuta ina mganga au nesi mmoja,siku akipeleka ripoti au kwenda benki kilomita 60 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ile Zahanati inafungwa na hakuna huduma inayotolewa,sasa ndugu zangu ugonjwa hauna taarifa haujui umepeleka ripoti,niombe serikali mkija mtuambie mkakati ambao mmeupanga,”ameomba.

ELIMU.

Upande wa elimu ameomba upatikanaji wa walimu 1,380 ili kukidhi upungufu uliopo.

“Sisi katika halmashauri ya Ikungi tuna upungufu wa walimu wengi sana ukiangalia hesabu yetu tunahitaji 2,685 lakini tunao 1,305 tu maana yake tuna upungufu wa 1,380,leo tunataka ufaulu upande lakini hatuwezi kupandisha ufaulu huo bila ya kuwa na walimu wakutosha,na katika hali hii tusitegemee mapinduzi ya elimu katika nnchi yetu,”amesisitiza.

Amesema idadi ndogo ya walimu inashindwa kukidhi uwiano wa walimu na wanafunzi ambapo baadhi ya shule za msingi unakuta kuna walimu watano kwenye shule yenye watoto zaidi ya 700.

“Tunashukuru tumeweza kupata fedha kwenye shule shikizi kule Simbikwa,Taru Mlimani,Mau,Mbughantigha,leo hii tumepanga tusajili shule zianze kufanya kazi lakini zina mwalimu mmoja au wawili,hivyo tusitegemee mabadiliko makubwa ya kitaaluma katika shule zile ,niombe sana tuisaidie idara ya elimu ipate walimu wa kutosha ili afisa elimu anaposimamia awe na uwezo mzuri wa kuelekeza namna serikali inavyotaka kuboresha elimu ,”ameongeza.

Amekumbusha ahadi iliyotolewa na Katibu Mkuu TAMISEMI Prof.Riziki Shemdoe ya kutoa fedha kwa ajili ya kupaua shule ya Msingi Kipompo iliyojengwa kwa juhudi za wananchi.

“Kule Kipompo Prof.Shemdoe uliahidi kukutoa fedha kwa ajili ya kupaua shule hiyo,sasa tayari wananchi wameshajenga madarasa manne pamoja na nyumba ya walimu tunasubiri upauaji ili shule hiyo isaidie wananchi ambao watoto wao wanatembea kilomita tisa kutoka kitongoji cha Kipompo Kata ya Mang’onyi,”ameongeza.

Amesema katika mwaka mmoja huo Halmashauri ya Ikungi wamepokea zaidi ya Sh Bilioni saba.

“Fedha hizi za maendeleo ni nyingi na tunaona zipo katika meneo mbalimbali ya vijiji vyetu,tumeona jambo kubwa la kujenga madarasa 67 na tulipata Shilingi Bilioni 2.6 ni fedha nyingi kwa wakati mmoja, tunashukuru sana na tunaipongeza serikali kwa mapinduzi makubwa katika elimu kenye halmashauri yetu,”amebainisha.

Mtaturu amezungumzia pia suala la ujenzi wa Chuo cha Veta Ikungi ambapo kukamilika kwake kutatoa fursa ya vijana kupata ujuzi na kuweza kujiajiri.

“Niishukuru serikali tulitengenewa fedha Shilingi Bilioni mbili kujenga Chuo cha Veta,lakini ninapoongea na wewe ule ujenzi umesimama,watu wa Veta walipewa kandarasi ya kujenga chuo, nashukuru Naibu Waziri Elimu alikuja akabadilisha utaratibu akasema uende halmashauri hivi ninavyoongea umerudishwa tena Veta,

Ameongeza kuwa,“Hivi ninavyoongea sasa wakandarasi hawajalipwa,mradi umesimama,vifaa hakuna na zaidi ya mifuko ya saruji 1,800 iliyokuwa inaenda Ikungi imepotea njiani haijafika,ujenzi umesimama hakuna kinachoendelea,vijana hawa tunaowatarajia wapate elimu hakuna mahala pa kufundishwa,hivyo tusitegemee mabadiliko ya kielimu au kusababisha ajira kwa wananchi wetu,”amesema.

BARABARA.

Mtaturu ameomba kuwe na mpango maalum wa kujenga madaraja na vivuko ili kusaidia barabara zinazojengwa vijijini ziweze kukamilika kwa wakati.

“Kwenye barabara tumepata Shilingi Bilioni 1.5 na imeleta mabadiliko makubwa na tunaipongeza serikali lakini kwa barabara za vijijini ambazo tunahitaji vivuko na madaraja, na bajeti hatutengi tutakuwa tunategemea kitu ambacho hatujakipanga,

“Ingekuwa vizuri fedha za maendeleo zinatoka moja kwa moja TARURA tunatenga kwa ajili ya vivuko na madaraja ili mameneja wa wilaya wabaki kwenye eneo la kutengeneza barabara na matuta,lakini ukisema leo afanye kazi ile ile usitegemee mabadiliko ya barabara katika halmashauri zetu,”amesisitiza.

PONGEZI.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake wameona maono na dhamira yake,“Kwa hakika tumeona huruma yake kwa ajili ya watanzania,”.

Amempongeza pia Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa na viongozi wengine wa wizara hiyo kwa hotuba nzuri iliyoonyesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tamisemi ndipo ambapo wananchi wapo wengi ndipo inatoa huduma nyingi kwa wananchi,ukiongelea Mamlaka za serikali za mitaa unaongelea wananchi wa vitongoji ,leo tumeona dhamira ya serikali katika eneo hili,hongera waziri Bashungwa unatoa ushirikiano kwa wabunge,na kero zilizo katika maeneo yetu mnazitatua kwa wakati,”ameeleza.

About the author

mzalendoeditor