Featured Kitaifa

TUME YA MADINI YAENDELEA KUNADI UBUNIFU, UKUSANYAJI WA MADUHULI YA SERIKALI

Written by mzalendoeditor

Watumishi wa Tume ya Madini nchini wametakiwa kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na tozo mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili kuvuka malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa ambapo kwa sasa mchango wa sekta ya Madini ni asilimia 7 katika pato la Taifa.

Wito huo umetolewa kupitia mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya kwenye kikao cha wahasibu na maafisa fedha cha siku tatu kilichoanza mapema juzi jijini Dar es Salaam chenye lengo la kukusanya taarifa kwa ajili ya kuandaa taarifa ya pamoja ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kuweka mikakati ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema kuwa Tume ya Madini imekuwa na historia ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yanayopangwa kwa kila mwaka ambapo kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 Tume ilipanga kukusaya shilingi bilioni 470 na ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 527 sawa na asilimia 111 ya lengo, mwaka 2020/2021 Tume ilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 526 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 584 sawa na asilimia 111.3 ya lengo na kusisitiza kuwa mikakati mbalimbali inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa lengo la ukusanyaji wa maduhuli la shilingi bilioni 650 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 linafikiwa.

” Mikakati iliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na ukusanyaji wa madeni ya nyuma kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini pamoja na kutoa elimu kwenye maeneo yenye shughuli za madini,” amesema Mtinya.

Ameongeza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha ukaguzi kwenye madini ujenzi kwa kuongeza rasilimali watu kwenye vituo vya ukaguzi wa madini ya viwanda na ujenzi ili kuhakikisha kodi stahiki zinalipwa.

Katika hatua nyingine ameongeza kuwa Tume imeanzisha mfumo wa kieletroniki wa ulipaji wa kodi mbalimbali za madini ya viwanda na ujenzi ambapo jumla ya Tsh billion 35 zinategemewa kukusanya kwa njia ya kielekroniki (POS), lengo likiwa ni kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa maduhuli

About the author

mzalendoeditor