Featured Kitaifa

KITUO CHA UWEKEZAJI CHANADI MAFANIKIO YA KITUO NDANI YA ROBO TATU YA MWAKA 2022

Written by mzalendoeditor

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeweza kupata mafanikio makubwa katika robo tatu ya mwaka inayoanzia Januari mpaka Machi, 2022 kutokana na ongezeko la usajili wa miradi na kuimarika kwa shughuli za uratibu na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kupitia utoaji wa huduma mahala pamoja ndani ya TIC.

Mafanikio yamepatikana kupitia uhamasishaji uwekezaji na kuhudumia wawekezaji hapa nchini ambapo katika kipindi cha robo mwaka ya tatu usajili wa miradi mipya ya Uwekezaji imefanyika.

Katika kipindi cha mwezi Januari hadi tarehe 31 Machi 2022 jumla ya miradi 85 imesajiliwa ikilinganishwa na miradi 51 iliyosajiliwa katika kipindi hicho mwaka 2021 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 66.7 miradi iliyosajiliwa katika kipindi hicho inatarajiwa kuzalisha ajira 12,191 ukilinganisha na ajira 4772 zilizoripotiwa kipindi hicho mwaka 2021 ambalo ni ongezeko la asilimia 155.47.

 

Upande wa mitaji, miradi iliyosajiliwa katika kipindi hicho ina thamani ya Dola za Marekani milioni 787.40 ikilinganishwa na kipindi hicho mwaka 2021 ambapo thamani ya miradi ilikuwa dola milioni 450.56 ambalo ni ongezeko la asilimia 74.76.

Miradi hiyo ipo katika sekta za viwanda, usafirishaji kilimo, ujenzi/majengo ya biashara, miundombinu ya kiuchumi, Taasisi za fedha, rasilimali watu, usafirishaji, utalii na huduma (Service). 

Kituo pia kimepokea miradi muhimu ambayo imeanza utekelezaji ambapo mradi wa TAQA Arabia Tanzania Limited ni mradi muhimu unatarajiwa kupunguza makali ya uingizwaji wa bidhaa za petroli kwani utaanzisha ujenzi wa vituo 12 vya ujazaji gasi ambapo ndani ya mradi huo kutakuwa na maeneo ya ubadilishaji wa magari (conversion centres) ambapo magari binafsi, ya abiria, malori na magari makubwa (heavy duty trucks) yatabadilishwa kutoka kutumia petroli na diseli kwenda kutumia gesi. Mradi uko katika hatua ya utekelezaji na inatarajiwa vituo viwili vikubwa vitakuwa vimekamilika robo mwaka ya mwisho wa mwaka huu. Mradi huo utaleta ajira za moja kwa moja-160 na uwezo ni kilogramu 700,000 kwa mwaka za gesi na utekelezaji wake utakuwa na vituo 12 Dar-es-salaam nzima.

Katika kipindi cha robo tatu yamwaka kumekuwa na utiaji saini mikataba ya utekelezaji na wawekezaji wakubwa wa kimkakati sita (6) kwa pamoja ambayo inatarajia kuwekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.10 itatoa ajira za moja kwa moja zipatazo 28,710 na kuokoa fedha za kigeni zaidi ya dola za Marekani bilioni moja ambazo zingetumika kuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. Miradi hiyo ni pamoja na Itracom Limited wa uzalishaji wa mbolea, Bagamoyo Sugar Limited wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa Sukari, Kagera Sugar Limited ambayo imejikita kwenye Kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, Mtibwa Sugar Estates ni ya mradi wa Kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, Knauf Gypsum Limited inafanya shughuli za uzalishaji wa bidhaa za Gyspsum na Taifa Gas ambayo inafanya usindikaji wa gesi.

Kituo kimeendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje kwa kushirikiana na ofisi za kibalozi na ofisi za wakuu wa Mikoa. TIC bado imeendelea kupokea wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini. Hii imetokana na Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu wezeshi kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na umeme. Diplomasia ya uchumi pia imekuwa chachu katika kuifanya Tanzania kuwa kivutio katika kuwekeza barani Afrika.

Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuhamasisha Diplomasia ya Uchumi itasaidia katika kuinua na kufanikisha uhamasishaji wa Uwekezaji hapa nchini. Taswira nzuri inayofanywa kupitia ziara za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan zinaleta sura kuwa Tanzania ni sehemu bora na inayofaa kuwekeza.

Kituo cha Uwekezaji kinaendelea kuibua fursa za uwekezaji pembezoni mwa Reli ya kisasa (SGR). Mpaka sasa miradi nane (8) imefanyiwa uchambuzi yakinifu kwa kushirikiana na UNDP. Hivyo, wawekezaji sasa wanaweza kuja kuwekeza katika miradi hiyo. Miradi nane iliyofanyiwa upembuzi yakinifu ni pamoja na uzalishaji chakula cha mifugo, usindikaji wa maziwa, Mvomero, uandaaji na upimaji wa ardhi, uchimbaji wa mawe ya ujenzi, kiwanda cha nyama, uzalishaji/ unenepeshaji wa mifugo, Mvomero, huduma za kupaki magari na uzalishaji wa mimea ya kulishia mifugo, shamba la Vikunge.

Kupitia TIC Serikali imeendelea kufanya maboresho ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha Kituo cha utoaji wa huduma za mahali pamoja “One Stop Facilitation Centre ya TIC”. Uundwaji wa mfumo wa kuunganisha mifumo ya Taasisi zote ili kuwa na Dirisha Moja la Kutoa Huduma za Vibali na Leseni kwa Wawekezaji Kimtandao (TeIW) unaendelea mjini Morogoro.Dirisha la Pamoja la kuhudumia Wawekezaji la Kielektroniki Tanzania (TeIW) ni suluhisho la mtandao ambalo linalenga kuwezesha na kurahisha upokeaji wa maombi, utoaji wa huduma za vibali, leseni na usajili kwa wawekezaji kwa haraka.  

Serikali imechukua hatua ya kutumia teknolojia ya mawasiliano na kuweka vigezo vinavyotumika kutoa huduma. Kupitia Kituo cha Uwekezaji imerahisisha mfumo wa utoaji cheti cha Uwekezaji kwa kufanya maboresho mtiririko wa nyaraka na mafaili, utoaji maamuzi wenye tija. Mwanzo mwekezaji alikuwa anapitia mtiririko wa hatua 44, kwa sasa ni hatua 13 mpaka kupata Cheti cha Uwekezaji.

About the author

mzalendoeditor