Featured Kitaifa

JESHI LA UHIFADHI LAANDIKA HISTORIA MPYA TAWA

Written by mzalendoeditor

  
Na Mwandishi Wetu, TAWA

KWA mara ya kwanza katika historia ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), inayotekeleza mfumo wa Jeshi la Uhifadhi, imepata maafisa wapya 17 wa vyeo vya Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Kamishna Msaidizi, wanaokwenda kuongeza tija katika utendaji wa Mamlaka maeneo mbalimbali nchini.

Kupandishwa vyeo kwa viongozi hao, kumekuja baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, kupitisha uamuzi huo katika kikao chake cha 20, kilichofanyika hivi karibuni mkoani Arusha, ambapo kati ya hao 17, watano (5) ni Makamishna Wasaidizi Waandamizi na 12 ni Makamishna Wasaidizi.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika leo katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA, Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali (mstaafu), Hamis Semfuko pamoja na kuwapongeza, amewaagiza maafisa hao kuwafahamu vizuri maafisa wengine na askari walio chini yao ikiwemo uwezo wao, ili wajue namna bora ya kuwaongoza.

Meja Jenerali mstaafu Semfuko aliongeza kuwa, kila afisa aliyevalishwa cheo kipya leo, anapaswa kuijua kikamilifu nchi, uongozi wake na siasa zake, ili kumudu nafasi wanazokwenda kuzitumikia.

“Jueni mambo ya taifa hili, uongozi wake na siasa zake, kiujumla tunatarajia mabadiliko makubwa katika utumishi wenu.

“Huko katika vituo vyenu, hatutarajii kuwe na migogoro, hatutarajii kusikika uvamizi wa wananchi hifadhini na hatutarajii unyanyasaji wa wananchi wala rushwa,” amesema Meja Jenerali Semfuko.

Amewaagiza maafisa hao kuishi vizuri na wananchi walio jirani na maeneo ya hifadhi na kusimamia askari wa uhifadhi, ili watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria na nidhamu za kijeshi.

Kadhalika amesema Bodi ya TAWA imepandisha vyeo vya maafisa hao kwa uwazi na weledi wa hali ya juu na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa kila mtumishi mwenye sifa za kupandishwa cheo kazini.

Meja Jenerali Semfuko pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro ambaye hivi karibuni alihamishwa na Rais Samia Suluhu kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, kwa uongozi wake mahiri uliosababisha TAWA kupata mafanikio makubwa.

“Pia nitumie fursa hii kumpongeza Waziri wetu wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunaahidi kumpa ushirikiano pamoja na taasisi zote anazosimamia ili kazi zote za uhifadhi zifanyike kwa maslahi ya taifa na vizazi vya sasa na vijavyo,” aliongeza.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, akizungumza katika maelezo yake ya awali, alisema uteuzi wa viongozi hao waliovalishwa vyeo vipya umefanyika kwa mujibu wa Muundo wa Shirika na Amri za jumla za jeshi la Uhifadhi, amri namba 5 kwa kuzingatia fani, uwezo wa kuongoza, uadilifu na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Bodi ya TAWA kwa kwa uteuzi wa viongozi hao, kwamba una umuhimu kwa sababu unalenga kufanya ugatuzi wa majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na Makao Makuu kwenda kwenye ngazi ya Kanda.

“Usimamizi imara katika ngazi ya Kanda utaimarisha uwezo wa Mamlaka kuhudumia wateja na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi,” amesema.

Mabula amesisitiza kuwa, menejimenti ya TAWA itafanya kila linalowezekana kuzijengea uwezo Kanda za Uhifadhi ili kutekeleza majukumu kadiri yaliyoelekezwa katika muundo wa Mamlaka hiyo.

About the author

mzalendoeditor