Featured Kitaifa

MSAFARA WA WAENDESHA BAISKELI WA TWENDE BUTIAMA WAFIKA JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

Msafara wa Baiskeli wa Twende Butiama ukiwasili katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma. Msafara huo wa waendesha baiskeli hao unaelekea Butiama katika kuadhimisha miaka 100 ya Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Waendesha Baiskeli wa Twende Butiama wakiwa pamoja wasanii wa kikundi cha Julius Nyerere Festival wakiimba nyimbo za hamasa mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma leo Jijini Dodoma tarehe 8 Aprili 2022.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma Mkomi akizungumza mara baada ya kupokea Msafara wa Baiskeli wa Twende Butiama ulipowasili katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma ukielekea Butiama, Mkoani Mara katika kuadhimisha miaka 100 ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dk.Christowaja Ntandu,akizungumza mara baada ya kupokea Msafara wa Baiskeli wa Twende Butiama ulipowasili katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma ukielekea Butiama, Mkoani Mara katika kuadhimisha miaka 100 ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mkuu wa Msafara wa Baiskeli wa Twende Butiama Bw. Gabriel Landa akielezea lengo la msafara huo ulioanzia Msasani nyumbani kwa mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam mpaka Butiama  katika kuadhimisha  miaka 100 ya Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma Mkomi na viongozi wa Wizara hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na waendesha baiskeli wa Twende Butiama katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo mtumba Jijini Dodoma.

…………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

WIZARA ya Maliasili na Utalii,imewapokea wachezaji  27 wa   timu ya    waendesha baiskeli ya Twende Butiama pamoja na Wasanii wa Maigizo,Jijini Dodoma   ambao wataendesha baiskeli kwa zaidi ya Kilomita 1500 mpaka Butiama Mkoani Mara  kwa ajili ya   kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa  Hayati Mwalimu Julius Kambarage.

Msafara huo umepokelewa   leo Aprili 8,2022 Makao Makuu ya Wizara hiyo Mtumba Jijini Dodoma   na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Juma Mkomi pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Mkuu wa msafara huo,Gabriel Landa amesema safari hiyo itakuwa ni ya siku tano na  wameianza   jana Jijini Dar es salaam na walilala Gairo na leo wamefika Jijini Dodoma na wanatarajia kulala Itigi Mkoani Singida.

Amesema  kesho safari yao wataanzia Itigi mpaka Nzega na kisha Nzega mpaka Magu na watamalizia Magu mpaka Butiama.

“Safari kama hizi tumeanza tangu  mwaka 2018 lengo   ni kushirikiana na Wizara katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa kutimiza miaka 100 kama angekuwa hai.Nitoe shukrani kwa Wizara kuendelea kuenzi yale mazuri ambayo yamefanywa na mwalimu Nyerere,”amesema.

Mkuu huyo wa msafara pia amesema wamekuwa wakihamasisha utalii  ambapo wamewahi kwenda Ngorongoro,Mikumi na Kolo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Mkomi amesema kwao ni furaha kupokea timu hiyo ya waendesha baiskeli ambapo amewapongeza kwa moyo wao wa kujitoa kwa vitendo katika kuenzi mambo mazuri ambayo yamefanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Wametembea na baskeli kwa sababu wakati huo baiskeli ilikuwa ni muhimu na ilikuwa ikitumika kufikisha ujumbe.Wizara ya Maliasili na Utalii itaratibu zoezi hili mpaka kilele Aprili 13 Butiama.

Amesema  wameamua kushiriki tukio la kuenzi yale yote ambayo ameyafanya na Baba wa Taifa kwasababu alikuwa ni muhifadhi namba moja wa vivutio vya Utalii nchini.

Kwa upande wake,Msanii wa Maigizo,Ahmed Olotu maarufu kwa jina la Mzee Chilo amesema kumuenzi Mwalimu Nyerere ni jambo muhimu kwani kuna baadhi ya vijana hawaelewi amelifanyia nini Taifa.

“Mataifa makubwa kama China wanawaenzi viongozi wao hata hapo Afrika Kusini na wao wanamuenzi Nelson Mandela kwanini isiwe sisi mimi na wenzangu tutaendelea kutangaza mazuri ambayo yamefanywa na Mwalimu Nyerere,”amesema.

Naye Mwigizaji Korongo Hamis Maarufu kwa jina la Mzee Korongo amesema watamuenzi mwalimu Nyerere kwa kusema yale mazuri ambayo aliyafanya ili jamii iweze kujua.

Naye,Veronika Godfrey   amesema atashindwa kumalizia mbio hizo kutokana na kupata maumivu ambapo amedai hiyo ni mara yake ya pili kushiriki huku akiwahamasisha wanawake kujitokeza kushiriki mchezo wa mbio za baiskeli.

About the author

mzalendoeditor