Featured Michezo

CAF YAKUBALI OMBI LA SIMBA SC KUINGIZA MASHABIKI 60 ROBO FAINALI DHIDI YA ORLANDO PIRATES

Written by mzalendoeditor

SHIRIKISHO  la Soka barani Afrika (CAF) limekubali ombi la Klabu ya Simba kuingiza Mashabiki Elfu 60 (60,000) katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Aprili 17, 2022 majira ya Saa 1:00 usiku katika dimba hilo la Kumbukumbu ya jina la Mzee wa Lupaso, Benjamin Mkapa. Pia mchezo huo unatarajiwa kuwepo kwa teknolojia ya ‘Video Assistant Referee’ (VAR) ikiwa ni kwa mara ya kwanza kutumika nchini Tanzania.

Shirikisho la Soka nchini (TFF) imetoa taarifa ya CAF kuteua Waamuzi na Maofisa wengine watakuwepo nchini kwa ajili ya mchezo huo mkubwa. TFF imesema CAF imeteua Mwamuzi wa Kati Haythem Guirat kutoka Tunisia, Mwamuzi Msaidizi namba moja ni Khalil Hassani kutoka Tunisia, Mwamuzi Msaidizi namba mbili ni Samuel Pwadutakam kutoka nchini Nigeria na Mwamuzi wa Akiba, Sadok Selmi kutoka Tunisia.

Mwamuzi wa teknolojia ya VAR, Ahmad Elghandour kutoka Misri na Mwamuzi Msaidizi Youssef Elbosaty kutoka huko huko nchini Misri.

Katika hatua nyingine, mchezo wa Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Azam, uliokuwa uchezwe Aprili 13, 2022 kati ya Simba SC dhidi ya Pamba FC umesogezwa mbele ili kuipa Simba SC nafasi ya maandalizi ya mchezo huo wa Robo Fainali ya CAF CC.

About the author

mzalendoeditor