Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa akifunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Aprili 06, 2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa akimkaribisha Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa kufunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Aprili 06, 2022 jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akitambulisha wageni na wajumbe wa kikao kazi cha maafisa Utamaduni na Michezo wakati wa kufunga kikao kazi cha 13 Aprili 06, 2022 jijini Dodoma.

Kikundi cha ngoma cha Makunga kutoka kijiji cha Nzali wilaya ya Chamwino kikitumbuiza wakati wa hafla ya kufunga kikao kazi cha maafisa Utamaduni na Michezo 13 Aprili 06, 2022 jijini Dodoma.

Baadhi ya maafisa Utamaduni na Michezo wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa kufunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Aprili 06, 2022 jijini Dodoma.

…………………………………………………

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Dodoma

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Innocent amewaelekeza watendaji wote wanaohusika na utekelezaji wa mabadiliko ya muundo wa kada za Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo ulioidhinishwa kutekelezwa haraka iwezekanavyo ifikapo Julai 01, 2022.

Waziri Bashungwa amesema hayo Aprili 06, 2022 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo ambapo amehimiza maandalizi ya utekelezaji wa muundo huo mpya yaanze sasa ili kutoa huduma kwa wadau wa sekta hizo na Watanzania kwa ujumla.

Akifunga kikao kazi hicho, Waziri Bashungwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia kuanzishwa kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumuagiza Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa kuanzishwa Kitengo hicho kipya cha Utamaduni, Sanaa na michezo kwa kuwa ni kitengo muhimu kama vitengo vingine nchini ambapo lengo lake ni kuwahudumia Watanzania katika sekta hizo.

“Niwahakikishie, maelekezo ya Waziri Mkuu aliyayatoa hapa wakati wa kufungua kikao kazi hiki tutayatelekeza pamoja na Maazimio yanayohusu utekelezaji kwa upande wa TAMISEMI naahidi yatafanyiwa kazi na kutolewa taarifa kila baada ya miezi minne kama ilivyo kwa taasisi nyingine ili tunapokutana katika kikao kazi kingine, tuwe na taarifa ya jumla ya utekelezaji na tusonge mbele zaidi” amesema Waziri Bashungwa.

Katika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Bashungwa amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kukaa mara moja na kuchambua maelekezo ya Waziri Mkuu ili yafanyiwe kazi kwa wakati kwa manufaa ya kuwahudumia Watanzania nchi nzima.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake inashirikiana kwa karibu na OR-TAMISEMI katika kutekeleza majukumu na maelekezo ya viongozi ili kufikia azma ya Serikali.

“Tunaenda kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji katika Wizara hii, kila mmoja wetu aende kuchapa kazi tukawape furaha Watanzania, nendeni mkawe wanyenyekevu na muwe karibu na wananchi ili tufanikishe malengo ya Serikali. Jengeni mahusiano mazuri na wananchi ili tufanye mapinduzi ya kiutendaji katika sekta hizi muhimu kwa nchi, hii ni Wizara ya raha na starehe” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa Wizara hiyo ni nguvu laini (soft power) ya nchi, hivyo maafisa hao wametakiwa kuweka uzalendo na utaifa mbele ili sekta hizo ziweze kuwa na tija kwa taifa na wananchi wake kwa maendeleo endelevu.

Kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo ni cha 13 tangu kuanzishwa kwake 2009 na kinajumuisha maafisa hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara pamoja na halmashauri zote nchini ambapo mwaka huu kimefanyika kwa siku tatu kuanzia Aprili 4-6, 2022 kwa kufunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Previous articleMIRADI YA UWEKEZAJI YA SH. TRILIONI 18.58 YASAJILIWA NCHINI-MAJALIWA
Next articleTUME YA HAKI ZA BINADAMU YAIPONGEZA SERIKALI KWA KURIDHIA MAPENDEKEZO 187

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here