POLISI mkoani Morogoro, imewatia mbaroni watu watatu wakituhimiwa wizi vifaa vya mapambo mbalimbali ya sherehe za Jeshi la Magereza.
Vifaa hivyo viliibwa wakati vikisafirishwa katika gari yenye namba za usajili T.644 BAK, aina ya Canter kutokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Fortunatus Musilimu amewataja watuhumiwa hao ni Emmanuel John maarufu kwa jina la Kaberebenze (27), mkazi wa Kihonda Mbuyuni, Manispaa ya Morogoro, Dickson Deus (23) maarufu Mavivian, mpiga debe wa gari za Mikese na Omari Saidi (32) wote wakazi wa Mikese, Morogoro.
Kamanda Musilimu amesema Machi 24, saa tisa usiku, dereva Fred Jackon (42) mkazi wa Sinza, Dar es Salaam, akiendesha gari hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma, alisimamishwa na dereva mwezake eneo la Mkambarani, wilaya ya Morogoro, barabara ya Dar es Salaam- Morogoro.
Amesema aliposimama dereva mwenzake, alimjulisha kuwa huko atokako kuna watu wameshusha mizigo kwenye gari yake.
Kamanda Musilimu amesema dereva huyo alipokagua, aligundua kuwa baadhi ya mizigo haipo na ndipo akatoa taarifa kituo cha Polisi Kingolwira, Manispaa ya Morogoro.
Amesema Polisi walianza ufuatiliaji na Machi 26, mwaka huu, saa tisa alasiri eneo la Kihonda Mbunyuni, Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro, Polisi walipokea taarifa za kiintelejensia za kuwepo kwa mzigo wa maturubai na vitambaa vya rangi mbalimbali vya kupambia vilivyoibwa.
Amesema walifanya upekuzi kwenye nyumba wanapoishi watu hao, walizikuta mali hizo za wizi na kuwakamata watuhumiwa wawili.
Amesema watuhimiwa hao walikutwa na mali hizo ambazo ni maturubai manne meupe, mabango matatu yenye picha za Rais na vitambaa 59 vya mapambo vyenye rangi ya bendera ya Tanzania na kwamba mali zote zimetambuliwa na dereva huyo.
Amesema katika kuendelea na ufuatiliaji zaidi, Machi 31, mwaka huu, saa nne usiku eneo la Kihonda Mbuyuni, Manispaa ya Morogoro, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine Omari Said (32) na wote wanahojiwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.