Na Marco Maduhu, SHINYANGA
WANAFUNZI 238 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini, wamehitimu Rasmi mafunzo yao ya ufundi katika fani tofauti, ambazo walikuwa wakisoma katika chuo cha ufundi Stadi Veta mkoani Shinyanga.
Mafunzo hayo ni Programu Maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, ambayo yalitolewa kwa ajili ya kukuza ujuzi kwa vijana, ambayo ni ya kozi fupi na yalianza kutolewa June mwaka jana na kuhitimishwa Desemba, huku mafunzo kwa vitendo yakimalizika Machi 6 mwaka huu.
Makamu Mkuu wa Chuo cha ufundi Stadi Veta Shinyanga Magu Mabelele, akitoa taarifa ya Programu hiyo maalum ya kukuza ujuzi kwa vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema walipokea maombi ya vijana 1,400 lakini mahitaji yalikuwa ni 280 ambao ndiyo walianza mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali, ambapo 42 hawakumaliza na kuhitimu 238.
Alisema anaishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo kwa vijana katika kuwajengea ujuzi na kukichagua chuo hicho cha Veta Shinyanga, ambacho pia kimejitangaza na kuhamasisha wazazi wengine kupeleka watoto wao chuoni hapo.
Alisema kwa mafunzo waliyopata vijana hao chuoni hapo kwa sasa wameshaiva na hata kujiajiri wenyewe, ambapo katika mafunzo yao wameweza kufanya mambo makubwa mengi ikiwamo na kufunga mfumo wa umeme katika chuo cha Veta Igunga.
“Kutokana na vijana hawa jinsi walivyoiva naweza kutembea kifua mbele kwa kuzalisha vijana wazuri, hivyo naomba Serikali katika utekelezaji wa miradi yao mbalimbali ya ufundi iwatumie vijana hawa wapo vizuri hata utengenezaji wa viti, meza, na madawati ya shule za hapa Shinyanga baadhi wametengeza wenyewe na
Awali katika Risala ya wanafunzi hao iliyosomwa na Mariam Said, waliipongeza Ofisi ya Waziri kwa kuwafadhili mafunzo hayo, ambayo yamewapatia mwanga wa maisha na kwenda kutimiza ndoto zao.
Walisema katika mafunzo hayo wamefanikiwa pia kushiriki kujenga chuo cha Veta Kishapu na Igunga,,kukarabati mfumo wa umeme chuo cha Veta Shinyanga, kutengeza viti, meza na madawati Seti 1,650 kwa shule za Msingi na Sekondari Manispaa ya Shinyanga.
Waliongeza kuwa wamejenga darasa moja chuo cha Veta Shinyanga, pia wametengeza Pete na Hereni kwa kutumia madini ya Vito, kushona sare za wanafunzi ngazi ya tatu chuoni hapo.
Aidha, walisema kutokana na kupata mafanikio hayo makubwa, changamoto kubwa ambayo wanaiona kuwakabili ni ukosefu wa mitaji ambayo itawawezesha kujiajiri wenyewe, na kuiomba Serikali kupitia mikopo ya Halmashauri asilimia Nne kwa vijana, iwapatie kwa urahisi ili wajiajiri na kupata vipato na kuendesha maisha yao.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi, alitoa wito kwa vijana hao kuwa ujuzi ambao wameupata kwenye mafunzo hayo wakautumie vizuri kujiajiri, pamoja na kuendelea kuchangamkia fursa za mikopo ya halmashauri ili wapate mitaji.
Alitoa wito pia kwa wazazi kwa wale wanafunzi ambao watajiunga tena na mafunzo chuoni hapo kupitia programu hiyo, wawaunge mkono kwa kuwapatia nauli za kwenda chuo pamoja na kuwatimizia mahitaji mengi ili wasikatishe mafunzo na kutimiza ndoto zao.
Katika hatua nyingine aliwataka wahitimu watakapo rudi majumbani mwao pia wakawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kuhesabiwa Sensa ambalo litafanyika Agosti mwaka huu, ili kuirahisishia Serikali katika mipango yake ya maendeleo kwa wananchi.
Mratibu wa mafunzo ya Programu hiyo ya kuwajengea vijana ujuzi Donald Bukombe, alitaja fani za ufundi ambazo wamesomea wanafunzi hao 238 kuwa ni umeme wa majumbani, ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, uashi, uchomeleaji na uungaji vyuma, ukataji na ung’arishaji madini ya vito, useremala na utengezaji wa vifaa vya umeme.
Alitaja idadi ya wanafunzi waliohitimu kuwa wapo 238, wavulana 135 na wasichana 103.