Jeshi la Polisi mkoani Geita  linamshikilia Renatus Christopher (31) dereva wa lori, T177AHH aina ya Isuzu kwa tuhuma za kumgonga na kumuua mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Nguzombili Geita mjini  wilayani Geita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Henry Mwaibambe amesema tukio hilo  limetokea leo majira ya saa tano asubuhi  jirani na makutano ya Barabara ya Mwatulole na Mwabasabi eneo ambalo lina shule mbili za Msingi yaani Mwatulole na Nguzombili.

Mwaibambe amemtaja mtoto huyo kuwa ni  John Frank mwenye umri wa miaka saba(7) amefariki dunia akiwa anakimbizwa hospitali kwa matibabu.

Kamanda Mwaibambe amwongeza kuwa Jeshi hilo limewasiliana na wakala wa Barabara za mjini na vijijini (Tarura) ambao ndio wasimamizi wa barabara hiyo kwa ajili ya kuweka alama za barabarani.

Amesema jeshi la polisi litasimamia uwekaji wa alama kwenye barabara hiyo (pundamilia na matuta) ndani ya siku mbili.

Aidha amesema kuwa kwasasa kabla ya Tarura haijaweka alama barabarani  Jeshi hilo litaweka askari wa Usalama barabarani ili kuhakikisha wanafunzi wanavuka kwa Usalama .

Mmoja ya mkazi wa eneo hilo, Neema Fabiano alitaja chanzo kikubwa cha ajali eneo hilo ni kutokuwepo kwa alama za barabarani hivo ni vyema serikali ichukue hatua za haraka.

Mwenyekiti wa Shule ya Msingi Nguzombili, Ngulu-Bright Tanganyika alieleza eneo hilo limekuwa na ajali za mara kwa mara kutokana na mqendokasi wa madereva wa malori hayo na kuomba serikali kuchukua hatua za kuweka matuta au alama za pundamilia ili wanafunzi hao wawe salama.

CHANZO:MWANGAZATV

Previous articleGEKUL KAZI YA UIGIZAJI INA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUHAMASISHA MASUALA YA KITAIFA, WAIGIZAJI WAOMBA CHAMA CHAO KUTAMBULIKA
Next articleTANZANIA YABANWA MBAVU NA SUDAN MECHI YA KIRAFIKI YA KIMATAIFA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here