NAIBU waziri wa utamaduni Sanaa na michezo Paulina Gekul akifungua  mkutano wa chama cha waigizaji Tanzania 
Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) Salum Mchoma  akiongea katika mkutano wao unaoendelea mkoani Arusha.
BAADHI ya wasanii wakifuatilia  jambo katika mkutano wao unaoendelea mkoani Arusha
……………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Naibu Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo,Pauline Gekul amesema kuwa fani ya uigizaji inamchango mkubwa kwa Taifa kwani imekuwa na washiriki wazuri hasa wa kusimama mstari wa mbele kwenye kuhamasisha masuala mbalimbali ya Taifa.
Sambamba na hayo wasanii wa sanaa ya uigizaji wameomba chama chao kutambuliwa na serikali  ili waweze kupata fedha za mikopo hasa asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuweza kuwasaidia kupata maendelo na kujikwamua kiuchumi.
Gekul aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) unaoendelea mkoani Arusha ambapo wameona wasanii wakifanya mambo makubwa hasa katika kampeni za kutokomeza majanga mbalimbali kama vile UKIMWI, UVIKO-19, vita pamoja na kuhamasisha jamii kufuata maadili.
Alieleza kuwa  kutokana na umuhimu huo Rais Samia Suluhu ameona umuhimu wa kufufua Mfuko wa  Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuwapatia zaidi ya bilioni 1.4 ili kuwania kiuchumi waigizaji nchini ambapo kupitia fedha hizo wanaweza kukopa kwa riba nafuu na kuendeleza kazi zao huku wakichangia kukuza uchumi wa Taifa na wao binafsi.
Aidha amewataka wasanii nchini kuwa mabalozi wazuri wa  wimbo wa Taifa, ili kuhakikisha hakuna mtu anayeweka vionjo vingine nje ya vilivyoasisiwa kwani kimsingi wimbo huo haupaswi kuchezewa kwa kuingiza vionjo au maneno mengine nje ya yaliyopo.
“Nawaomba nyie muwe mabalozi wa kulinda wimbo wetu huu ambao umeasisiwa na unaonyesha utaifa wetu,haifai kuongezewa madoido mengine  ambayo hayaleti maana kama ulivyoasisiwa na wasisi wetu, unapaswa kubaki na usajili wake,”Alisema Gekul.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) Salum Mchoma aliiomba serikali kupitia TAMISEMI kuwatambua na kuweza kuwapa mikopo kama mitaji kazi zao ili kuweza kujikwamua kiuchumi lakini pia kulipeleka taifa mbele zaidi katika Sanaa ya uigizaji.
Pia alisema kuwa chama hicho kinawachama hai 36,714  ambapo wanamahitaji mbalimbali, kwani uigizaji ni rasilimali na kazi yao kubwa   kuikumbusha serikali na jamii kuwa sanaa ni muhimu katika uchumi wa nchi.
“Tanzania inazaidi ya wasanii milioni 6 kati yao wasanii milioni 3 wanatokana na kazi za uagizaji lakini hatupo pamoja, hivyo vema serikali ikatukusanya pamoja ili  kutusaidia kutambulika, kuwa kitu kimoja kwa maslahi mapana ya nchi yetu,”alieleza.
“Tunaomba maafisa utamaduni watupokee vivyo hivyo ili tusikwame kimaendeleo pia tunaomba kupunguziwa na kuondolewa kodi na tozo ya kazi kwa wasanii ili  tusiwe na mzigo mkubwa wa gharama za kazi zetu,”alisema.
Naye Msemaji wa Yanga na balozi wa kampuni ya GSM,Haji Manara alitoa rai kwa wasanii nchini kutumia  misingi ya Azimio la Arusha kwaajili ya kujikwamua kiuchumi kwani hali iliyopo hivi sasa kwa wasanii si ya kuridhisha kutokana na baadhi yao kuwa na majina makubwa lakini uhalisia wa kimaisha duni.
Alisema kuwa mkutano huo uwe chachu ya kujikwamua kiuchumi kwa wasanii kuwa na maslahi bora na kujikwamua kiukwasi kutokana na kazi zao ambapo GSM imewasaidia  wasanii kutoa vifaa mbalimbali kwaajili ya watu wenye uhitaji katika Hospitali ya Mount Meru ikiwemo kutoa fedha kwaajili ya kusaidia chama hicho cha wasanii kukua kiuchumi.
Mwenyekiti wa  chama cha waigizaji Mkoa wa Arusha,Fredrick Kephace  wamesema mkutano huo umewakutanisha wasanii waigizaji zaidi ya 150 kutoka mikoa 22 nchini.
“Lakini mikakati tuliyonayo kama Chama ni kuhakikisha wanawainua waigizaji mmoja mmoja pamoja na makundi hivyo wanatafuta wafadhiri na tayari wapo kwenya mazungumzo na baadhi ya wadau kuhakikisha  tunafanya filamu  ambazo zitatuinua na kufikia hatua za kimataifa,”alisema Mwenyekiti Kephace.
Previous articleRAIS SAMIA AFANYA UTEUZI
Next articleAJALI:LORI LA MCHANGA LAUA MWANAFUNZI DARASA LA KWANZA GEITA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here