WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 28,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

WATUMISHI wa Wizara na Waandishi wa Habari wakifatikia hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima (hayupo pichani),leo March 28,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 28,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

………………………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk.Doroth Gwajima ametaja vipaumbele 15  ambavyo wamepanga kuvitekeleza kwa mwaka 2022-2023.

Dk.Gwajima ameyasema hayo leo Machi 28,2022 jijii Dodoma  wakati  akitaja mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja  amesema vipaumbele vyao ni pamoja kuratibu afua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee.

Pia,Kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo,Kuratibu wafanyabiashara wadogo (Machinga) ili kuboresha mazingira ya biashara zao,Kufanya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha jamii kubadili mtazamo na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa ajili ya wanawake na makundi mbalimbali katika jamii kujiajiri.

Vilevile,Kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali, mikopo yenye masharti nafuu na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia wezeshi,Kuingiza masuala ya jinsia katika Sera, Mikakati, Mipango, Miongozo na Bajeti za Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mtaa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia.

“Kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi na nafasi mbalimbali za maamuzi,Kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum wakiwemo  manusura wa majanga mbalimbali,Kuimarisha mifumo ya malezi, ulinzi na maendeleo ya watoto na familia,Kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa haki na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto,”amesema.

Pia,Kuratibu utekelezaji wa huduma jumuishi za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Watoto kwa watoto katika umri wa miaka 0-8,Kuratibu utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (2021/22 – 2024/25),Kuratibu utekelezaji wa Ajenda ya Malezi (Parenting Agenda 2019 – 2030) ijulikanayo kama “Familia Bora Taifa Imara.

Vilevile, Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii naKuimarisha ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika katika Maendeleo ya Taifa.

WAMACHINGA

Amesema Serikali imewatambua rasmi Wamachinga kuwa Kundi Maalum ambapo tarehe 22-23 Februari 2022, Wizara iliandaa semina elekezi iliyofanyika  Jijini Dodoma ikijumuisha viongozi 10 wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) ngazi ya Taifa pamoja na viongozi 78 kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Amesema  lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya uongozi, ujasiriamali, ulipaji Kodi na utii wa sheria bila shuruti.

Aidha, katika kikao hicho Serikali iliweza kutoa ufafaunizi juu ya fursa zilizopo Serikalini na namna wanavyowezea kuzifikia na kuwanufaisha.

“Katika kuhakikisha shughuli zao zinaratibiwa vizuri, Wizara pia imewawezesha Machinga kupata Usajili wa Shirikisho la Umoja wao (SHIUMA), Ofisi ya Shirikisho hilo ngazi ya Taifa na Mkoa wa Dodoma,”amesema.

KIZAZI CHENYE USAWA

Waziri Gwajima amesema  chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania iliwasilisha ahadi za Nchi kuhusu kizazi chenye usawa kwenye mkutano wa kimataifa na kuchagua kuwa kinara katika eneo la pili la haki na usawa wa kiuchumi kati ya maeneo sita ambayo ni mahsusi katika Jukwaa hilo lililoasisiwa na Umoja wa Mataifa.

Amesema Rais ameshaunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri  yenye wajumbe 25 kutoka pande 2 za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).

Vilevile, Wizara ilifanikiwa kuratibu uzinduzi wa Kamati hiyo ya  Kitaifa ya Ushauri, Uratibu na Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Ahadi za Nchi Kuhusu Kizazi chenye Usawa (Generation Equality Forum – GEF).

Amesema Uzinduzi huo ulifanyika Dodoma Desemba  16 mwaka jana  ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi na mafanikio katika utekelezaji wa ahadi hizo ambazo Nchi  iliahidi kuhusu haki na usawa wa kiuchumi kwa Wanawake.

Amesema Serikali kupitia Wizara hiyo inaandaa Mpango wa Utekelezaji wa Miaka 5 kwa ajili ya Programu ya Kitaifa kuhusu Kizazi chenye Usawa itakayotekelezwa kwa mfumo wa ushirikishwaji kupitia ushiriki wa Serikali, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu, Asasi zisizo za Kiraia, Wadau na Washirika wa Maendeleo na Mashirika Yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa ili kufikia Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake.

MAKAO MAKUU WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI

Dk.Gwajima  amesema Makao hayo yamejengwa katika eneo la Kikombo nje ya mji wa  Dodoma kwa ufadhili wa Shirika la Abbott Fund kwa thamani ya Shilingi Bilioni 12.7 yenye uwezo wa kutoa huduma kwa watoto 250.

Amesema hadi kufikia Februari 2022, jumla ya Watoto 55 (Ke 21 na Me 34) wanapatiwa  huduma za msingi, marekebisho ya tabia na stadi za maisha kwa ajili ya kuwaandaa kujitegemea hapo baadaye, kuwaunganisha na familia zao na kuwapatia malezi mbadala ikiwa pamoja na malezi ya kambo au kuasiliwa.

Amesema Serikali imeandaa mazingira wezeshi kwa Taasisi na Sekta Binafsi kwa ajili ya kusajili na kuendesha makao ya Watoto katika mikoa tofauti.

“Makao ya watoto nchini yaliyosajiliwa yameongezeka kutoka 130 mwaka 2015/16 hadi kufikia 214 mwaka 2020/21 yakiwemo Makao mawili (2) yanayomilikiwa na kuendeshwa na Serikali ambayo na (Makao ya Watoto Kurasini – Dar es Salaam na Kikombo – Dodoma),”amesema

UKATILI WA KIJINSIA

Dk.Gwajima amesema katika kukabiliana na matukio ya vitendo vya ukatili kwenye Taasisi za Elimu ya juu na kati, Serikali kupitia Wizara iliandaa Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Madawati ya Jinsia katika Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati.

Amesema lengo likiwa kuweka mfumo wa kushughulikia matukio ya unyanyasaji wa kingono na vitendo vya ukatili katika maeneo ya vyuo ambapo hadi kufikia Februari 2022, jumla ya Madawati saba yameanzishwa katika Taasisi za Elimu.

 Amvitaja vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Iringa, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya cha Bugando.

MTAKUWWA

Amesema Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA 2017/18 2021/22).

Waziri Gwajima amesema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 1,843 zimeanzishwa na kufanya idadi ya kamati za hizo kufikia 18,186 kati ya Kamati 20,750 zilizokusudiwa kuanzishwa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa ifikapo Juni 2022. Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa watoto kuhusu namna ya kujilinda na vitendo vya ukatili kupitia Mabaraza ya Watoto pamoja na kablu za watoto mashuleni ili kuongeza uelewa na kusaidia katika kutoa taarifa endapo mtoto huyu atafanyiwa ukatili.

Vilevile, Serikali imeweka  walimu wa unasihi katika shule za msingi na Sekondari ambao wanatumika kama moja ya njia ya kutoa elimu kwa watoto kuhusu vitendo vya ukatili na kuwasaidia Watoto kuibua vitendo vya ukatili ambavyo wanafanyia shuleni au nyumbani ili kuwasaidia.

“Serikali imeendelea kufanya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa lengo la kutoa elimu na kueneza uelewa kwa wananchi juu ya kupinga na kutokomeza Vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia nchini,”amesema.

VIJANA BALEHE

Waziri Gwajima amesema katika kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma rafiki za afya na kuondoa vikwazo kwa Maendeleo ya Vijana Balehe nchini Serikali inatekeleza  Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe nchini (2021/22 – 2024/25).

Amesema ajenda hiyo  imejikita katika nguzo sita  ambazo ni  Kuzuia Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, kutokomeza mimba za Utotoni,Kuzuia Ukatili wa Kimwili, Kisaikolojia na Kingono, Kuboresha Lishe, Kuhakikisha Watoto wa Kike na Kiume wanabaki shule.

Amesema katika kuimarisha malezi na makuzi jumuishi ya watoto kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu CCM Kifungu 93 (c); Serikali imeandaa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/22 – 2025/26) yenye lengo la kumlea mtoto wa umri wa miaka 0 – 8 ili kufikia utimilifu wake.

Aidha, Wizara imejenga Vituo Jumuishi vya Kijamii vya Kulelea Watoto (Community-Based Early Childhood Development Centers) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu hiyo.

Amesema vituo hivyo vina lengo la kutoa huduma jumuishi za Malezi na Makuzi kwa watoto walio na umri kuanzia miaka 2 hadi chini ya miaka 5  kwa kuwapatia huduma jumuishi za afya, lishe, ulinzi, ujifunzaji na uchangamshi wa awali kabla ya kujiunga na darasa la awali.

Amesema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, jumla ya Vituo vya mfano 30 vimejengwa katika Mikoa ya Dar es Salaam (10) na  Dodoma (20).

HAKI ZA WATOTO

Waziri Gwajima amesema katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa watoto wanaokinzana na sheria sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu CCM Kifungu 93, Serikali  imefanya ufuatiliaji  katika magereza yaliyopo mikoa ya Rukwa, Katavi, Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Amesema ufuatiliaji huo umewezesha watoto 16 kuachiwa huru kutoka Gereza Kuu la Segerea na kuwekwa chini ya uangalizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, watoto watano  wametolewa Gereza Kuu la Segerea na wamehamishiwa Mahabusu ya watoto Upanga.

MSONGO WA MAWAZO

Aidha, amesema katika kuimarisha huduma za ushauri na msaada wa kisaikolojia kwa familia na jamii kwa watu wenye misongo ya mawazo, manusura wa vitendo vya ukatili pamoja na migogoro ya ndoa na familia (Ilani ya Uchaguzi Mkuu CCM Kifungu 93 (L) Serikali imeanzisha huduma za usuluhishi na msaada wa kisaikolojia kwa njia ya mtandao.

Amesema  hadi kufikia Februari 2022, jumla ya wahitaji 203 walihudumiwa ili kuimarisha mahusiano katika familia, ndoa na jamii kwa ujumla.

Aidha, Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Dar es Salaam imeanzisha Kituo cha Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa lengo la kutoa huduma kwa wanafunzi, wafanyakazi na wanajamii.

MABARAZA YA WAZEE

Amesema Serikali imekamilisha uundaji wa Mabaraza ya Wazee katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kisha kuunda Baraza la Taifa la Wazee na hivyo kufikia lengo la kuwa na Mabaraza 20,749. Vilevile, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee Nchini (2018/19-2022/23) ikiwa ni pamoja na kufuatilia afua zinazotekelezwa katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa wazee. Lengo ni kutokomeza mauaji ya wazee nchini ifikapo mwaka 2023. Jitihada hizi zimesaidia kupunguza mauaji ya wazee kutoka 190 mwaka 2015 hadi 54 kufikia Februari, 2022.

Vilevile, katika kuimarisha huduma za matibabu kwa Wazee, Serikali imeendelea kuwatambua wazee wasiojiweza na kuwapatia vitambulisho vya msamaha wa matibabu.

Amesema Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021, wazee 758,498 (475,252 Me na 283,246 Ke) wametambuliwa ambapo wazee 508,595  sawa na asilimia 67 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF).

Aidha, Serikali imeunda timu za uratibu na usimamizi wa huduma katika Hospitali na Vituo vya Afya  nchini ili kutoa usaidizi na kuhakikisha wazee wanapata huduma. Timu hizo zinajumuisha wataalam watatu (3) ambao ni Daktari, Muuguzi na Afisa Ustawi wa Jamii.

MASHIRIKA YASIYOKUWA YA KISERIKALI

Amesema Katika kuimarisha ushirikiano wa Serikali na Wadau, Wizara imeanzisha jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa ajili ya kujadili utendaji kazi na mchango wa mashirika katika maendeleo ya nchi lililozinduliwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Septemba, 2021 Jijini Dodoma.

Amesema sambamba na  uzinduzi wa jukwaa hilo, Taarifa ya Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2020 ilizinduliwa ambayo ilibainisha kuwa Shilingi Trilioni 1.1 zilitumika katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, hifadhi ya jamii, uwezeshaji kiuchumi, utawala bora na mazingira.

MWELEKEO

Amesema mwelekeo wa Wizara ni pamoja kuwa na kizazi chenye usawa sambamba na maendeleo ya makundi mahsusi ya jamii tuliyokabidhiwa ambayo ni watoto, wanawake, wajane, wazee, na machinga.

Pia,kuimarisha uratibu wa kisekta kwani dhana zote za maendeleo na ustawi wa jamii zinatekelezwa na kila sekta hivyo kuratibu ili sera na miongozo ya sekta hizi iakisi dhana ya maendeleo na ustawi wa jamii kwa usawa wa kijinsia na kuzingatia makundi maalumu.

“Kuwezesha upatikanaji wa raslimali wataalamu waliowezeshwa ili jamii ipate huduma ya kutosha ya wataalamu wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii sambamba na kuinua upya kasi ya tasnia ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwani ni tasnia za msingi sana kwenye maendeleo ya sekta zote.

“Kuhakikisha tunawezesha jamii kufahamu, kumiliki na kutekeleza kwa weledi dhana ya maendeleo ya jamii kwa jamii kuwa na uendelevu kwenye kujenga fikra chanya za maendeleo na kuepuka yote yanayorudisha nyuma maendeleo na ustawi wa jamii hususan ubaguzi na ukatili wa kijinsia,”amesema.

Previous articleTIMU YA BIG TIME YAIBUKA KIDEDEA  KIPANGA CUP
Next articleRAIS SAMIA ATETA NA WAZIRI MKUU MSTAAFU WA UINGEREZA TONY BLAIR IKULU CHAMWINO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here