Featured Kitaifa

HOSPITALI YA KIBONG’OTO YAIBUA WAGONJWA 306 WA TB KLINIKI TEMBEZI

Written by mzalendoeditor

Na.WAF-Mererani

Hospitali Maalumu ya Tiba ya Magonjwa Ambukizi-Kibong’oto imeweza kuwaibua wagonjwa 306 wa Kifua Kikuu katika maeneo mbalimbali ya machimbo nchini Katika kipindi cha mwezi Julai -Desemba 2021.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt.Leonard Subi wakati wa maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani yaliyoadhimishwa kwenye mgodi wa Mererani .

Dkt. Subi amesema kuwa kwa kutumia kliniki tembezi waliweza kuwafikia wananchi zaidi ya 8600 katika maeneo mbalimbali ya machimbo nchini Tanzania.

“Wagonjwa hao tuliowaibua tuliwaanzishia matibabu mara moja na kama tusingewaibua wangeweza kuambukiza watu wengine “Alisema Dkt.Subi

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka miundombinu mizuri ya matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu,huduma za uchunguzi, matumizi ya teknolojia za kisasa za ugunduzi wa Kifua Kikuu kwa kutumia mashine za ‘Gene xpert’ ambazo hutoa majibu ya ‘TB’ ndani ya saa mbili mpaka tatu tofauti na zamani ambapo ilikua ni zaidi ya siku tatu.

Kwa upande wa hospitali ya Kibong’oto Dkt.Subi amesema zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa wa TB waliolazwa katika hospitali hiyo wanatoka maeneo ya wachimbani madini na zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa hao wanatumia hewa tiba ya oksjeni.

“Wagonjwa wengi wa maeneo ya wachimbaji wanaathiriwa na vumbi la madini na hivyo huwaathiri mapafu na wengi walio katika hatari ni wachimbaji wadogo hivyo tunayo sababu ya kuunganisha nguvu katika kupambana na TB”Alisisitiza

Hata hivyo aliwataka Wizara ya Madini, Wamiliki wa Migodi na Wadau Mbalimbali kuelimisha wachimbaji wadogo, wakubwa na wakati, wamiliki wa migodi pamoja na kusimamia sheria mahala pa kazi ili kudhibiti magonjwa ya mapafu yanayotokana na vumbi aina ya silica(Silicosis) na maambukizi ya TB.

Dkt.Subi alisema ushiriki wa sekta zote ni muhimu kwenye mapambano dhidi ya TB na kuwakumbusha wananchi endapo atamuona mtu mwenye dalili za Kifua Kikuu kumshauri kwenda kwenye kituo cha kutoa huduma za afya kilicho karibu kupata ushauri,uchunguzi na matibabu kwani TB inatibika na matibabu yake ni bure kwenye vituo vyote nchini

About the author

mzalendoeditor