Featured Kitaifa

WAFANYAKAZI WA WIZARA MNA DHAMANA YA KUIPELEKA TANZANIA KIDIJITALI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Habari Mawasiliano, Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatina alipowasili katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kufungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi.

Waziri wa Habari Mawasiliano, Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye(kulia) akifurahia jambo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi baada ya Waziri huyo kuwasili katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kwa ajili ya kufungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Waziri wa Habari Mawasiliano, Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Machi 25,2022 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Machi 25,2022 jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatina akizungumza kwenye mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari uliofanyika  leo Machi 25,2022 jijini Dodoma.

Mwenyekiti TUGHE wa Tawi la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Laurencia Masigo akizungumza wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Machi 25,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (aliyesimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Wizara hiyo baada ya kufungua mkutano wa baraza hilo uliofanyika leo Machi 25,2022 jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi

………………………………………………………………

Prisca Ulomi na Faraja Mpina, WHMHT, Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka wafanyakazi wa Wizara anayoiongoza kutambua kuwa wao ni sehemu ya kuipeleka Tanzania Kidijitali kwa kuwa wana wajibu, majukumu na dhamana ya kutekeleza sera, sheria, kanuni, miongozo na miradi ya kitaifa ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Waziri Nape ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika jijini Dodoma ambalo ni baraza lake la kwanza kulifungua tangu ameteuliwa kuongoza Wizara hiyo ambapo amewaarifu wajumbe wa mkutano huo kuwa watambue wao ni kiungo muhimu kati ya Menejimenti ya Wizara na wafanyakazi hivyo ni vema kiungo hicho kusimamiwa vizuri kwa kuwa Wizara hiyo inaangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu kuliko Wizara nyingine kuendana na dhamana ambayo imepewa ya kuipeleka Tanzania kidijitali

Ameongeza kuwa wafanyakazi hao ni sehemu ya Tanzania tunayoitaka na kutoa wito kwa Menejimenti ya Wizara kuhakikisha inaweka mazingira mazuri mahala pa kazi ili wafanyakazi waweze kutekeleza vema majukumu yao huku akiyataja baadhi ya majukumu ambayo Wizara imepewa ikiwa ni pamoja na kuziwezesha Sekta nyingine ambapo bila kuziwezesha zingesimama mathalani kupitia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao umejengwa na kufikia kilomita 8,319; utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwenye mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo anwani hizo zilikuwa zijengwe kwa miaka mitano lakini sasa utekelezaji wake unafanyika kwa miezi mitano; pamoja na utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali

“Mimi ni muumini wa haki kwa kuwa maisha niliyopitia yamenifundisha, tujifunze kutenda haki, ukiona kwenye moyo wako huwezi kutenda haki, Wizara hii sio mahali pako, wewe utaona haki ni jambo dogo ila kwa anaedai haki kwake ni jambo kubwa kwa kuwa linagusa maisha yake na haki atakayotendewa inaweza kuokoa maisha ya mwanae hivyo niwatake viongozi na wafanyakazi tupendane kwa kuwa upendo unatibu na natambua kila mmoja ana changamoto zake na sio rahisi kutimiza kila hitaji lakini jibu ni upendo,” amesisitiza Waziri Nape

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amezungumzia utekelezaji wa anwani za makazi kuwa ni jukumu  kubwa la Wizara kwa sasa na kuwataka wafanyakazi kuona fahari kuwa sehemu ya utekelezaji kwa weledi na kuacha historia kwa kuwa utekelezaji wa mfumo huo utaifungua nchi kuingia kwenye uchumi wa kidijitali 

Amewaeleza wajumbe wa baraza hilo kuwa Ofisi yake ni ofisi yao, iko wazi muda wote na amewataka wajisikie amani kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuzingatia uwajibikaji wa pamoja, amani na upendo katika kutimiza wajibu wa kila mmoja wao na kusisitiza kuwa nia njema hujenga mahusiano mema na utendaji wenye ufanisi  

Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatina amepongeza uongozi wa Wizara kwa kutimiza takwa la kisheria na kufanya baraza la wafanyakazi na ametoa rai kwa wafanyakazi wengine wajiunge na chama cha wafanyakazi cha TUGHE pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kujali maslahi ya wafanyakazi nchini

Naye Mwenyekiti wa Tawi la TUGHE wa Wizara hiyo akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo, Laurencia Masigo amesema kuwa anashukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kujali wafanyakazi na kwa sasa hawana malalamiko wala hoja iliyowasilishwa kwenye uongozi wa Baraza hilo ambapo hii inadhihirisha kuwa mahali pa kazi kuna amani, umoja na ushirikiano  na kufanya kazi katika timu moja ndio nguzo ya mafanikio

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza hilo, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samwel Nyungwa amesema kuwa wamefarijika kuona wapo pamoja na Waziri Nape kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi kwa kuwa imeonesha kuwaheshimu na kumuahidi kama ulivyowaheshimu wanaenda kuchapa kazi kama alivyoelekeza kwa kuzingatia Waziri Nape ndio amebeba taswira ya Wizara hiyo hivyo watahakikisha taswira hiyo inaendelea kung’aa 

Mkutano wa Baraza unafanyika kwa siku mbili jijini Dodoma ambapo wajumbe watapitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya mwaka wa fedha 2021/2022; na mpango wa bajeti wa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023

About the author

mzalendoeditor