Featured Kitaifa

DC ARUMERU ATOA  SAA 27 WANANCHI KUONDOA MAZAO KWENYE CHANZO CHA MAJI CHA MOIVARO.

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mhandisi Richard Ruyango Akizindua zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji cha Moivaro.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mhandisi Richard Ruyango akipanda mti katika chanzo cha maji cha Moivaro

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mhandisi Richard Ruyango akiongea na wananchi katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji cha Moivaro.

Mboga aina ya Saladi ikiwa imepandwa katika chanzo cha maji cha Moivaro.

…………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.

Mkuu wa ya Arumeru mhandisi Richard Ruyango ametoa saa 27 kwa wananchi wa kitongoji cha Moivaro kijiji cha Shangarai kata ya Ambureni kuondoa zao la mboga aina ya Saladi waliyoyapanda katika chanzo cha maji ya chamchem  ikiwa ni pamoja na waliojenga nyumba ndani ya eneo la chanzo hicho kubomoa ndani ya mwezi mmoja kuanzi leo Machi 25,2022.
Ruyango alitoa wito huo wakati alipokuwa akizindua zoezi la upandaji miti 1500 katika chanzo cha maji cha Moivaro kilicho chini ya usimamizi wa bodi ya bonde la Pangani ambapo 
alieleza kuwa uharibifu wa vyanzo haukubaliki hivyo wote wanaofanya shugli za kibinadamu waondoe hadi ifikapo kesho saa nane mchana.
“Chanzo kina maji mengi lakini wananchi wanapanda Saladi, wengine majani ya kulisha mifugo na kujenga pia hii haukubaliki kesho saa nane nitakuja kukagua kama mmeondoa na kusafisha chanzo hiki na nikikuta hamjafanya hivyo tutafanya wenyewe na wale wenye shughuli hizi tutaondoka nao hatua za kisheria zikafuatwe lakini pia mliojenga ndani ya eneo la chanzo nawapa mwezi mmoja muondoe nyumba zenu,”Alisema Mhandisi Ruyango.
Alifafanua kuwa miti 1500 waliyoipanda katika chanzo hicho itasaidia kufanya kiwe endelevu  na kwa halmashauri hiyo wanavyanzo 156 tofauti na maeneo mengine lakini wapo watu wachache wanaoharibu  jambo ambalo hawatalikubali kwani wakivitunza vitaendelea kuwepo na kama halmashauri kwa mwaka 2021 wamepanda miti 1600 na kwa mwaka huu wa 2022 wameshapanda miti 725 ambapo lengo ni kufikia miti milioni 1.5.
“Nawasihi wananchi miti tuliyoipanda leo ikawe ishara ya kutunza chanzo hiki, ondoeni haya mazao, fungeni mifugo yenu msiache ikiwa inazurura hovyo lakini pia kila mtoto apewe mti wa matunda apande na kuitumza hii itasaidia kuja kuwa na kizazi kitakachojali na kutunza mazingira ikiwemo vyanzo vya maji,” Alisema Mhandisi Ruyango.
Kwa upande a wake Mhandisi wa mazingira kutoka bonde la Pangani Malegeri Joseph akitoa taarifa ya chanzo alisema kuwa maji yanayotoka eneo hilo yanatumika katika matumizi mbalimbali lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo watu kufanya shughuli za kilimo ndani ya chanzo, ujenzi, ukataji miti pamoja na uchepushaji wa maji bila kufuata utaratibu.
Naye Kaimu mkurugenzi wa bodi ya  bonde la Pangani Godwin Kapama alieleza kuwa kampeni hiyo ya upandaji miti ni endelevu na litaendelea hadi msimu wa mvua utakapoisha ambapo wanalengo la kupanda miti zaidi ya laki moja katika vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo ndani ya bonde la Pangani.
Alisema kuwa chanzo hicho kumekuwa na changamoto nyingi ambazo wamekuwa wakipambana nazo kwa muda mrefu ambapo wameona katika zoezi hilo la upandaji miti ni muhimu wakaanza na eneo hilo ili waweze kukihifadhi vizuri.
Naye diwani wa kata ya Ambureni Faraja Maliaki alisema kuwa wamepokea maagizo ya mkuu wa wilaya na watayatekeleza ambapo wataanza zoezi la kuondoka mboga zilizopandwa ndani ya chanzo pamoja na kutunza miti lakini pia  amewataka wananchi  kuona kuwa ni wajibu wa kila mmoja kutunza chanzo hicho na mazingira kwa ujumla.

About the author

mzalendoeditor