Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kabla ya kufungua rasmi Daraja la Tanzanite lenye urefu wa Kilometa 1.03 pamoja na Barabara zake unganishi zenye urefu wa Kilometa 5.2 kuanzia eneo la Agha Khan (Barack Obama Road) hadi eneo la Coco Beach, katika hafla iliyofanyika eneo la Agha Khan Jijini Dar es Salaam.
…………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ujenzi wa daraja jipya la Selander (Tanzanite) ni muendelezo wa jitihada za Serikali kuimarisha miundombinu ili kukabiliana na kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya ufunguzi wa daraja hilo la Tanzanite lenye urefu wa kilomita 1.03 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2 iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Maandalizi ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka yanaendelea kutoka katikati ya Jiji kwenda Gongolamboto, nyengine kwenda Tegeta, pia kutoka Ubungo hadi Bandarini, Kigogo kwenda Tabata Dampo hadi Segerea na kutoka Morocco kwenda Lugalo hadi Kawe.
Rais Samia amesema, dhamira ya Serikali ni kuifanya Dar es Salaam kuwa Jiji la kisasa na la kipekee, kusaidia kupunguza foleni pamoja na kuwa kichocheo cha ukuaji wa shughuli za uchumi na biashara Jijini humo.
Vile vile, Rais Samia ameeleza kuwa ujenzi wa barabara na madaraja unagharimu fedha nyingi, hivyo kuwasihi wananchi kutunza miundombinu.
Rais Samia amesema Serikali inafanya jitihada za kuimarisha miundombinu katika miji mingine nchini, ikiwemo Jiji la Dodoma ambapo inajengwa barabara ya mzunguko ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya mji huo.
Gharama za ujenzi wa Daraja hilo la Tanzanite ni Dola za Kimarekani Milioni 123.032 ambazo ni fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Dola za Kimarekani Milioni 4.233 ikiwa ni mchango kutoka Serikali ya Tanzania.