Kutoka kulia ni Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi. Riitta Swan, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Fredrick Onael Shoo pamoja Msahuri wa Haki za watoto kutoka nchini Finland Bi. Anna Halmstrom wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Afya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Paul Mmbando akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Fredrick Onael Shoo, Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi. Riitta Swan pamoja na viongozi wengeni wa kanisa hilo uliofanyika leo tarehe 24/3/2022 jijini Dar es Salaam.

………………………………………………..

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) imeipongeza serikali kwa kuendelea kutetea haki za binadamu kwa kutoa fursa kwa watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua, huku wakitoa wito kwa Baraza la Kimataifa kuendelea kutoa ushirikiano katika kusaidia nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Kanisa la KKKT ni wadau wa Haki za Binadamu mbele ya Baraza la Kimataifa ambapo imeelezwa kuwa katika sekta ya afya na elimu inatoa mchango mkubwa, huku ikibainishwa kuwa katika Afya hapa nchini inachangia asilimia 15 ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 24/3/2022 jijini Dar es Salaam Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Fredrick Onael Shoo, amesema kuwa serikali ya Tanzania katika jambo la haki za binadamu hasa wanawanake na watoto inafanya vizuri.

“Tunaipongeza serikali kwa kutoa fursa kwa watoto wa kike kuendelea na masomo bila kuwanyanyapaa, kwani wapo wanawake wengi waliopata ujauzito na walipopata tena fursa ya kuendelea walifika hadi elimu ya juu” amesema Dkt. Shoo.

Dkt. Shoo ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanatakiwa kuendelea kuchukua hatua kwa kila mtu anayefanya unyanyasaji kwa watoto wa kike na kiumbe pamoja na kupinga mila potofu ikiwemo unyanyasaji wa kingono na ndoa za utotoni.

Mkurugenzi wa Afya Kanisa la KKKT Dkt. Paul Mmbando, amesema kuwa kila mmoja anajukumu la kuhakikisha watoto wanapata haki zao bila kubaguliwa.

Dkt. Mmbando amefafanua kuwa kanisa halipendi kuona watoto wanapata mimba za utotoni, ila kwa jicho la huruma linapinga kuwanyanyapaa.

“Tutaendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa sababu wengi wanapata mimba bila kujijua, wanakuwa hawana ufahamu kuhusu mambo hayo” amesema Dkt. Mbando.

Msahuri wa Haki za watoto kutoka nchini Finland Bi. Anna Halmstrom, amesema kuwa serikali ya Finland imeweka sera ya kila mtu lazima aende shule jambo ambalo limefanikiwa na kuleta maendeleo.

Bi. Halmstrom amesema kuwa elimu ya uzazi nchini Finland inafundishwa kwa wanafunzi wote wenye umri kuanzia miaka 14 na kuendelea jambo ambalo limesaidia.

“Elimu ya uzazi ikitolewa ni jambo nzuri kwani nchi mbalimbali imewasaidia, mimi nimefanya kazi Tanzania kwa muda wa miaka 20 kupinga ukeketaji na ukiangalia kwa sasa ukeketaji umepungua tofauti na nchi nyengine” amesema Bi. Halmstrom.

Previous articleWAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UGANDA
Next articleWAZIRI NDALICHAKO ATETA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA DODOMA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here