Uncategorized

WAZIRI NDUMBARO ATAJA MAFANIKIO YA WIZARA YAKE KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 23,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa  waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 13,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

……………………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

WIZARA ya Maliasili na Utalii imetaja mafanikio 10 ambayo imeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

KUIMARIKA KWA UHIFADHI

Akiyataja mafanikio hayo mbele ya Waandishi wa Habari,Waziri wa Wizara hiyo,Dk.Damas Ndumbaro amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wizara hiyo imeweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuimarika kwa uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu.

Pia,Kanuni za jeshi la Uhifadhi zimepitishwa na kutambuliwa kuwa Jeshi kamili la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu.

Pia, Kupungua kwa ujangili ikiwamo kuuwawa kwa tembo na biashara ya pembe za tembo,Idadi ya faru, simba imeongezeka.

KUONGEZEKA KWA IDADI YA WATALII NA MAPATO

Amesema idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi pia iliongezeka kutoka watalii 562,549 mwaka 2020 hadi watalii 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2.

Vilevile, mapato yatokanayo na utalii wa ndani katika maeneo yaliyohifadhiwa yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 9.7 mwaka 2020 hadi Shilingi bilioni 12.4 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 27.8.

Alisema idadi ya watalii wa nje iliongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021,Mapato hayo yaliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 hadi milioni 1,254.4 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76.  

TUZO YA HESHIMA

Alisema Tanzania kutambuliwa na UNWTO kama nchi iliyostahimili na kufanya vizuri zaidi duniani katika utalii wakati wa janga la UVIKO-19, 2020 – 2021.

“Tripadvisor kupitia Travelers’ Choice Destination – Afrika imeziorodhesha Zanzibar na Jiji la Arusha kuwa miongoni mwa maeneo kumi bora ya shughuli za utalii Barani Afrika;

Pia, Tanzania ilichaguliwa na taasisi inayoandaa tuzo za utalii duniani (World Travel Awards – WTA) kuwa nchi inayoongoza kwa shughuli za utalii Barani Afrika (Africa’s leading destination for the year 2021).

“Tuzo ya Utalii wa Bara (Continental Tourism Award 2021) iliyotolewa na Bodi ya Utalii ya Afrika (African Tourism Board) wakati wa onesho la kwanza la EARTE lililofanyika Jijini Arusha Oktoba, 2021,”amesema.

FEDHA ZA UVIKO 19  

 Amesema Kutokana na juhudi za Rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi, tuliweza kupata mkopo wa fedha maarufu kama fedha za UVIKO-19.

Amesema kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, fedha hizo zimewezesha kukarabati miundombinu ya utalii ikiwemo barabara na madaraja katika maeneo ya Hifadhi.

KUFANYIKA KWA ROYAL TOUR

“Kama mnavyofahamu, kumekuwa na jitihada mahsusi za Mheshimiwa Rais katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu maalum ya Royal Tour.

Amesema  Kupitia program hiyo mtandao maarufu wa habari nchini Marekani wa theGrio umetambua juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuiongoza vyema sekta ya utalii nchini na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha kwanza cha utalii Afrika mwaka 2022.

“Hii imepelekea kuongezeka kwa watalii na wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo utalii,”amesema.

KUVUTIA WAWEKEZAJI

Amesema Mpango wa kutumia ndege za kampuni ya Emirates kutangaza vivutio vya utalii umesaidia kuongeza idadi ya watalii

Amesema kutumia timu za mpira wa miguu ikiwamo Atletico Madrid, Getafe, Real Valladolid Ajax na PSV kwa kutangaza vivutio vya Utalii katika viwanja vya timu zao kwa kuweka matangazo hayo katika mbao za viwanja hivyo.

KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

Amesema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wameweza kuenzi na kuthamini mchango wa Mwl. Nyerere katika kulitumikia Taifa la Tanzania.

Pia,kuchochea dhana ya uzalendo kwa wananchi hususani kwa vijana wanaochipukia katika Uongozi.

“Ikiwa ni pamoja na Kusheherekea miaka 100 tangu kuzaliwa kwake endapo angekuwa hai,”alisema.

UWEKEZAJI KATIKA VITALU VYA UWINDAJI

Amesema kumeendelea   kufanyika mnada wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya kielektroniki pamoja na kufanyika kwa uwekezaji mahiri katika uwindaji wa kitalii – SWICA.

MWENYEJI WA MIKUTANO YA KIMATAIFA

Amesema Tanzania itakuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 65 wa Utalii wa UNWTO kamisheni ya Afrika, Oktoba 2022.

Pia,Baraza la Utalii Afrika (Africa Tourism Council-ATC) limeichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wake mkuu utakaofanyika Zanzibar mnamo mwezi Septemba 2022;

KUENDELEZA SEKTA YA MISITU NA NYUKI 

Amesema wameweza kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu na kutengeneza bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu hapahapa nchini.

Pia,Kuanza kwa Programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki (BEVAC – Support to Beekeeping Value Chain Programme) utakaonufaisha wananchi wa mikoa saba ya Tanzania Bara na Zanzibar.

About the author

mzalendoeditor