Featured Kitaifa

JESHI LA POLISI KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI WAFANYA OPERESHENI YA KUTOKOMEZA AJALI ZA BARABARANI

Written by mzalendoeditor

 

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha

Katika kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kama sio kuisha kabisa Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani toka Makao makuu ya Polisi kimeendesha operesheni ya ukaguzi wa mabasi yanayobeba abiria katika stendi ya mabasi mkoa wa Arusha na kutoa elimu kwa madereva.

Akiongea na madereva wa mabasi yanayofanya safari zake toka mkoa wa Arusha kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania Mkuu wa Operesheni toka kikosi cha usalama barabarani Makao makuu Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Adam Maro ambaye ameongoza operesheni hiyo amewataka madereva kuacha tabia kuendesha mabasi kwa mwendo kasi kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Pia amewaasa kufanya ukaguzi wa vyombo vyao kabla ya kuanza safari ili kuepusha madhara ya ajali ambayo yanaweza kutokea kutokana na ubovu wa magari hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo amesema akiwa ni msimamizi wa sheria za usalama barabarani Mkoa wa Arusha hatakua na huruma wala kumuonea muhali dereva yeyote ambaye atafanya uzembe barabarani.

Naye Katibu wa Chama cha Kutetea abiria kanda ya kaskazini Bwana Godwin Mpinga amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Bwana George Joseph ambaye ni dereva ametoa wito kwa madereva wenzake kuhakikisha wanaendesha mabasi kwa kufuata sheria na kuacha tabia ya kusikiliza abiria wachahche wanaowashinikiza kutembea kwa mwendo kasi kwa lengo la kuwahi.

About the author

mzalendoeditor