Featured Kitaifa

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KUFANYA MABORESHO MRADI WA BWAWA LA CHAMAKWEZA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji wakati ilipotembelea Kijiji cha Chamakweza wilayani Chalinze mkoa wa Pwani kukagua ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo. Kushoto ni Mhe. Dkt. Chistina Ishengoma ambaye ndio Mwenyekiti wa Kamati hiyo. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Viongozi, Wataalam na Wafugaji wakati walipokuwa wanatembelea kukagua Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma (wa pili kutoka kushoto) akijiridhisha kama maji yanatoka kwenye bomba wakati Kamati hiyo ilipofika kukagua ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akitoa maelezo mafupi juu ya ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea mradi huo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akijibu baadhi ya hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa kikao kifupi kilichofanyika baada ya ukaguzi wa mradi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani kukamilika.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Viongozi, Wataalam kutoka Sekta ya Mifugo, Mkoa wa Pwani na Wafugaji wakisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge wakati wa kikao kifupi kilichofanyika baada ya kumalizika kwa ukaguzi wa mradi wa Bwawa la kunyweshea mifugo maji la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa wa Pwani.

………………………………………………

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Wizara itafanya maboresho kwenye mradi wa ujenzi wa Bwawa la kunyweshea maji mifugo Chamakweza ili liweze kutoa huduma iliyokusudiwa.

Waziri Ndaki ameyasema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea Kijiji cha Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani kukagua ujenzi wa mradi huo ambapo kamati ilibaini kuwepo kwa mapungufu katika utekelezwaji wa mradi huo.

Amesema kuwa mapungufu yaliyobainishwa na kamati hiyo yanatakiwa kufanyiwa maboresho ili mradi huo uweze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa kuhakikisha Mifugo inapata maji wakati wote.

Waziri Ndaki ameieleza kamati hiyo kuwa Wizara itajipanga upya katika utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja nakufanya mapitio ya mchoro na kuangalia namna ya utekelezaji wa ushauri na maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge.

Katika hatua nyingine Waziri Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kuunda timu ya wataalam itakayofuatilia namna mradi ulivyosanifiwa, utekelezaji wake na namna ulivyosimamiwa hadi kukamilika. Vilevile amemuagiza kumsimamisha kazi Mhandisi kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na timu ya uchunguzi itakayoundwa. Pia amemuagiza Katibu Mkuu amuandikie barua Katibu Mkuu Wizara ya Maji ili na yeye achukue hatua kwa wahandisi ambao walikuwa wanasimamia mradi huo unaotekelezwa katika mkoa wa Pwani.

Timu itakayoundwa kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa mradi ni lazima iwe imekamilisha taarifa hiyo ndani ya wiki moja na kuiwasilisha kwake ijumaa wiki ijayo, ambapo taarifa hiyo itawasilishwa siku hiyo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Aidha, Waziri Ndaki ameishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kuisimamia Wizara kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia sana katika kuboresha mazingira ya wafugaji hapa nchini na hivyo kuwafanya wafuge kwa tija kitu ambacho kutasaidia kuwaongezea kipato na kuongeza mchango wa sekta ya Mifugo kwenye Pato la taifa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dkt. Christina Ishengoma amesema kuwa kamati haijaridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo kwa kuwa kamati imebaini mapungufu ambayo yanasababisha mradi huo kutotoa huduma iliyokusudiwa.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa kamati imeielekeza Wizara kufanya maboresho katika maeneo yote yaliyobainika kuwa na mapungufu. Vilevile Wizara imetakiwa kuongeza Usimamizi kwenye miradi inayoitekeleza kwa kuwa baadhi ya wakandarasi wasio waaminifu wasioosimamiwa wanaweza tekeleza miradi chini ya kiwango.

Aloyce Ndakidemi ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo amewasihi wafugaji wa Kijiji cha Chamakweza kuulinda mradi huo kwa kuhakikisha Mifugo haiingii ndani ya bwawa. Ndakidemi amesema lengo la serikali ni zuri licha ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huo. Hivyo amewataka waendelee kuutunza mradi wakati serikali inajipanga kufanya maboresho kwenye mradi huo.

Mradi huu wa ujenzi wa bwawa la Chamakweza ulianza 19 Julai, 2020 na kukamilika tarehe 15 Mei, 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 671, Bwawa hilo linauwezo wa ujazo wa lita milioni 108,169,400. Kamati ya Kudumu ya Bunge imeishauri serikali kuhakikisha inayafanyia kazi mapungufu yote ambayo yamebainika katika utekelezaji wa mradi huo.

About the author

mzalendoeditor