Uncategorized

NAIBU WAZIRI SAGINI AWATAKA ASKARI POLISI KUTUMIA WELEDI NA MAADILI WANAPOTEKELEZA MAJUKUMU YAO

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Jumanne Sagini akipokea salamu ya heshima kutoka kwa askari Polisi wanaotarajia kuhitimu Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya cheo cha Koplo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Gwaride Kambapori,Shule ya Polisi Tanzania (TPS)Moshi,iliyopo Mkoani Kilimanjaro

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akikagua gwaride la askari Polisi wanaotarajia kuhitimu Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya cheo cha Koplo Kozi No. 4/2021/2022 katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi iliyopo Mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akikabidhi vyeti na zawadi kwa askari waliofanya vizuri katika Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya Cheo cha Koplo Kozi No.4/2021/2022 katika uwanja wa Gwaride Kambapori, Shule ya Polisi Tanzania(TPS) Moshi,Mkoani Kilimanjaro,

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akimvalisha Cheo cha Koplo wa Polisi mmoja kati ya askari waliohitimu mafunzo ya Uongozi mdogo ngazi ya cheo cha Koplo wa Polisi katika Shule ya Polisi Moshi, Kambi ya Kambapori iliyopo Mkoani Kilimanjaro

Naibu wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na askari Polisi wanaotarajia kuhitimu Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya cheo cha Koplo Kozi No. 4/2021/2022 katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi iliyopo Mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akiteta jambo na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Nchini, CP Liberatuss Sabas wakati wa Mahafali ya Kufunga Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya cheo cha Koplo katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, Kilimanjaro.

……………………………………………………………

Na Mwandishi MoHA,

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amewataka askari Polisi kote nchini kuendelea kutumia weledi, maadili na ushirikishwaji wa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kazi mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ninawaasa mtakapotoka hapa, mwende mkafanye kazi kama mlivyofundishwa, msifanye kazi kama mlivyozoea. Hakikisheni mnafanya kazi zenu kwa kufuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo na itakayokuwa ikitolewa na viongozi wenu. Alisema.

Naibu Waziri Sagini amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo wa cheo cha Koplo wa Polisi katika Shule ya Polisi, Kambi ya Kambapori Moshi,mkoani Kilimanjaro ambapo jumla ya askari 1751 wamehitimu mafunzo hayo.

Aidha amewaagiza askari hao kwenda kuyashughulikia makosa ya uhalifu wa kimtandao ambapo baadhi yamekuwa yakidhalilisha utu, kuchochea chuki na uhasama katika Jamii zetu pamoja na kuathiri uchumi na kutishia amani, utulivu na usalama. Amewasihi kuongeza kasi ya kujifunza sayansi na teknolojia ili kuongeza umahiri na weledi wa Jeshi la Polisi kuweza kuwa na mawasiliano ya haraka na Polisi wa mataifa mbalimbali kukabiliana kwa pamoja na uhalifu unaovuka mipaka, ukiwemo ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya madawa ya kulevya na mengineyo.

“Dunia ya sasa imekuwa kijiji, kuna mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, ambayo huweza kutumika vibaya. Kama wahalifu wanaungana kwa kutumia sayansi na teknolojia za kisasa, ni changamoto kwa Polisi wetu kuona haja ya kuungana kupitia teknolojia hiyo ili kudhibiti uhalifu

Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia na kuruhusu kupandishwa vyeo kwa maafisa, wakaguzi na askari wa ngazi mbalimbali wa vyombo vyote vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Waziri Sagini ameuagiza Uongozi wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kuzuia uhalifu na kuwashughulikia wahalifu wote watakaobainika hata kama ni maofisa, wakaguzi au askari wa Jeshi la Polisi.

“Nafadhaishwa na uwepo wa matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali na zaidi haturidhishwi kusikia kwamba wapo baadhi ya askari wanaosaidia au kushiriki katika uhalifu. Niutake Uongozi wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kuzuia uhalifu na kuwatia nguvuni wote wanaotishia usalama wa raia na mali zao.”

About the author

mzalendoeditor