Katibu Mkuu wa CCM Mhe.Daniel Chongolo akizungumza na waandishi wa habari katika kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani.
Katibu Mkuu wa CCM Mhe.Daniel Chongolo akisisitiza jambo katika kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani.Katibu Mkuu wa CCM Mhe.Daniel Chongolo akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari katika kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani.
Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM Bw.Shaka Hamdu Shaka katika akifuatilia kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani.Katibu Mkuu wa CCM Mhe.Daniel Chongolo akizungumza jambo na Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM Bw.Shaka Hamdu Shaka katika kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani. Katibu wa Nec Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Bw. Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga akifuatilia kikao maalumu cha CCM na waandishi wa habari kueleza Mafanikio ya mwaka mmoja wa Chama hicho ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Madarakani.
Baadhi ya maofisa mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi Makao Mkuu wakiwa katika mkutano huo uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndugu Daniel Chongolo.
Baadhi ya waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii wakifuatilia hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo.
PICHA EMMANUEL MBATILO
**********************
EMMANUEL MBATILO – DAR ES SALAAM
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleeza mafanikio waliyoyapata ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan ikiwemo ukuaji wa Uchumi kwa muda mfupi.
Akizungumza wakati akielezea mafanikio hayo Katibu Mkuu wa CCM Mhe.Daniel Chongolo amesema ukuaji chanya wa uchumi umeleta matokeo ya wazi yanayoonekana, mathalani kuongezeka kwa mzunguko wa fedha (ukwasi) kwa wastani wa asilimia 9.3, kutoka asilimia 4.8 iliyokuwepo mwaka wa fedha wakati Rais anakabidhiwa dhamana.
“Hii imesababishwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, msisitizo wa kuhakiki na kulipa malimbikizo ya madeni ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na hata wastaafu”. Amesema Mhe.Chongolo.
Amesema kumekuwa na nafuu kubwa upande wa mikopo chechefu kwa mabenki yetu nchini, ambapo imepungua kutoka asilimia 9.3 hadi sasa ni asilimia 8.2.
“Matokeo haya yamesababishwa na kuboreshwa kwa fursa anuai, ushikirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo na ulipaji wa malimbikizo ya madeni baada ya uhakiki kufanyika, hasa kwa wakandarasi”.Amesema
Aidha Chongolo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais samia kumeongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Kimarekani 60 bilioni hadi kufikia Dola za Kimarekani 64 bilioni.
“Kwa mujibu wa BoT, akiba hii inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua nusu mwaka. Wanasema pia, ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa EAC la miezi walau 4.5 na miezi 6 kwa wanachama wa SADC”. Amesisitiza Chongolo.
Pamoja na hayo amesema katika kipindi hiko cha mwaka mmoja, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeweka record ya kukusanya kiwango kikubwa cha mapato tangu kuanzishwa kwake kwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.5 mwezi Disemba mwaka jana.
“Mbali ya jambo hilo la kipekee, ndani ya kipindi hiki pia kumekuwa na ongezeko la mapato ya ndani kutoka shilingi trilioni 11.6 ya mwaka wa fedha wa 2020 – 2021, hadi kufikia shilingi trilioni 15.9, mwaka wa fedha 2021 – 2022, ikiwa ni sawa na asilimia 93.5 ya makadirio ya kukusanya trilioni 17.0. ongezeko hilo (shilingi trilioni 11.6-15.9) ni sawa na ongezeko la shilingi trilioni 2.1”. Ameeleza
Hata hivyo katika suala la elimu Chongolo ameeleza kuwa ndani ya mwaka huu mmoja wa uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, wanafunzi wa kidato cha kwanza wote wameingia shuleni kuanza masomo yao kwa siku moja bila kuwepo waliosubiria nyumbani kujiunga sekondari kwa chaguo la pili, ambalo miaka yote lilikuwa linasababishwa na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya (UPUNGUFU) miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, hasa vyumba vya madarasa na madawati.
“Hilo limewezekana baada ya kujengwa kwa madarasa 12,000, bila kusahau madarasa mengine 3,000 ya shule shikizi. Hiyo inafanya jumla ya madarasa 15,000 ambayo yalijengwa ndani ya miezi 3”. Amesema
Amesema kuna ujenzi wa shule zingine za sekondari mpya zipatazo 245 unaendelea, lengo likiwa ni kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Sekondari hususan kwa watoto wa kike, katika kata ambazo hazina shule za sekondari ili kuwapunguzia watoto umbali wa kutembea hivyo kuimarisha ulinzi wao waendapo na watokapo shuleni.
Hospitali za rufaa za mikoa 19 ziko katika hatua mbalimbali za kukamilisha ujenzi na ukarabati wake. Kuna miradi ipatayo 127 ya ujenzi wa hospitali inaendelea katika halmashauri za wilaya nchini, halikadhalika kuna ujenzi wa vituo vya afya vipatavyo 233 katika tarafa 207, vyote hivi vina uwezo wa kufanya upasuaji, vikiwa na majengo ya OPD, Maabara na vichomea taka. Bila kusahau ujenzi wa zahanati zipatazo 564 katika halmashauri mbalimbali nchini ambao uko katika hatua za kukamilika.
Kwenye suala la afya Chongolo amesema kuwa Katika eneo la upatikanaji wa dawa ili kuondokana na malalamiko ya wananchi, mbali ya Serikali kutumia takribani Shilingi bilioni 333 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendenashi, inajenga viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba katika eneo la Idofi, Halmashauri ya Makambako, mkoani Njombe kwa lengo la kupunguza ununuzi wa dawa kutoka nje ya nchi.
“Hatua hii itasaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununulia dawa nje ya nchi na hivyo fedha itakayookolewa itaelekezwa katika mipango mingine ya kuboresha huduma kwa wananchi”. Ameeleza.