Uncategorized

MVUA YAFANYA UHARIBIFU WA MAZAO CHAMWINO IKULU

Written by mzalendoeditor

Adeladius Makwega –DODOMA

Mvua kubwa ilionyesha ikiambatana na upepe mkali Jumatano ya Machi 16, 2022 Chamwino Ikulu imesababisha mahindi na alizeti kukatika na kuanguka katika mashamba kadhaa katika eneo hilo.

Mwandishi wa habari hii ameshuhudia mashamba ya baadhi ya wakaazi wa Chamwino Ikulu yakiwa na mandhari hiyo ya mahindi kuanguka chini yaliyosababishwa na mvua iliyodumu kwa saa mbili tangu saa 8 alasiri hadi saa 10 ya jioni.

Mandhari hiyo ilionekaka hata kwa maeneo yenye miti mingi matawi ya miti kama mikaratusi yakikatika chini kutokana mvua iliyoambatana na upepo mkali.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii wakaazi hao wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya chakufanya baada ya mahindi hayo kuanguka.

“Hapa siwezi kufanya lolote, je nitayaweza kuyaamsha mahindi haya yote na kuyawekewa udongo? Maana hapo itanibidi nimlipie mtu wa kufanya hivyo.” 

Alisema Mdala Anna, mkaazi wa Mtaa wa Talama, Chamwino Ikulu.

Mama huyu ambaye ni mtu mzima anasema kuwa mvua kama hii ilipaswa kunyesha wakati mahindi yakiwa madogo na ni ya faida kwa wale wenye mahindi madogo ambao si wengi.

“Hapa kinachoendelea ni kuyasimamisha na kuyawekea udongo japokua katika zoezi hilo mahindi kadhaa yanaweza kukatika na hapa mkulima ataingia hasara .” 

Alisema Mdala Maria ambaye alikuwa akiyatazama mahindi hayo wakati huo huku akiyawekea udongo.

Wakulima kadhaa wa Chamiwno Ikulu wamelima mazao mbalimbali katika kilimo mchanganyiko kama vile  mahindi, alizeti , karanga , kunde na maboga.

About the author

mzalendoeditor