Uncategorized

BILIONI 1.8 ZAFANIKISHA UJENZI DARAJA LA KISALALA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia) akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la Kisalala katika Mji Mdogo wa Laela jana linalojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.8 chini ya TANROADS.

Daraja la Kisalala katika barabara ya Laela- Mwimbi-Kizombwe linaloendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.89 chini ya mkandarasi mzawa M/s Mselem Civil Contractors wa Sumbawanga ambapo limefika asilimia 70 na litakamilika Aprili mwaka huu .

Meneja wa TANROAD Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga (kulia) akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa daraja la Kisalala jana wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Rukwa kukagua mafanikio ya utekelezaji Ilani.

Mafundi wa kampuni ya M/s Mselem Civil Engineering & Contactors ya Sumbawanga wakaiendelea na kazi ya ujenzi wa daraja la Kisalala lililopo Mji mdogo wa Laela.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Rainer Lukala akiwa na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa wakikagua mradi wa ujenzi wa daraja la Kisalala katika barabara ya Laela  hadi Kzombwe wilaya ya Sumbawanga jana.

Meneja wa TANROAD Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa CCM Rukwa Ndugu Rainer Lukala (kushoto ) wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kisalala  jana wilaya ya Sumbawanga lenye urefu wa mita 35 ambalo linajengwa kwa gharama za shilingi Bilioni 1.89 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

………………………………………………………….

Na. OMM Rukwa

Katika kuadhimisha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, Wakala wa Barabara mkoa wa Rukwa (TANROADS) umefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa daraja la kimkakati la Kisalala lenye urefu wa mita 35 litakalogharimu shilingi Bilioni 1.89.

Mafanikio hayo yameelezwa jana (16 Machi,2022)  na Meneja wa TANROAD Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa huo ilipokagua utekelezaji wa mradi huo katika kata ya Mnokola iliyopo Mji mdogo wa Laela wilaya ya Sumbawanga.

Mhandisi Mwanga aliongeza kusema Serikali ilitoa fedha mwezi Septemba 2021 ambapo mkandarasi mzawa M/s Mselem Civil Engineering and Contractors Company Ltd  wa Sumbawanga alipewa mkataba kwa gharama ya shilingi 1,890,117,000/- na kazi ilichukua miezi sita.

Meneja huyo wa (Wakala wa Barabara) TANROADs mkoa alisema daraja la Kisalala lina urefu wa mita 35 ambapo chanzo cha fedha ni Mfuko wa Barabara na kuwa tayari mkandarasi amelipwa shilingi 1,134,070,200/- huku kazi imefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi Bilioni 1.89 kwa kazi ya ujenzi wa daraja hili ambalo litakuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Kisalala  kuunganishwa  na maeneo mengine ambapo mradi huu utakamilika ,Aprili 16, mwaka huu” alisema Mhandisi Mwanga.

Kuhusu manufaa ya mradi huo, Mhandisi Mwanga alisema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa kiungo cha barabara kati ya Mji mdogo wa Laela na vijiji vya Mwimbi, Kizombe na nchi ya jirani ya Zambia.

Akizungumzia mradi huo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala alisema Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya  Mkoa imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa na wa kimkakati utakaokuwa mkombozi wa usafiri na uchumi wa wananchi wa Sumbawanga.

Lukala aliwataka wataalam wa TANROAD kuendelea kusimamia kazi za ujenzi wa barabara ili ziwe bora na ziakisi thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

“Kwa daraja hili kwa kulitazama tunaona michango mkubwa wa wakandarasi wazawa kufanikisha miradi na kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imetoa fedha nyingi kutatua kero za wananchi. Tanroad tuandalieni ziara ili tukaone mafanikio zaidi kwenye miradi ya miundombinu ili tuweze kuisemea vema kwa wananchi” alisisitiza Lukala.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema kazi ya ujenzi wa miundombinu kufungua maeneo yaliyojifunga inaendelea vema kutekelezwa na TANROAD pamoja na TARURA.

Kuhusu daraja hilo la Kisalala, Mkirikiti alisema ni muhimu kwani liko katika barabara inayoungaisha Sumbawanga na nchi ya Zambia hivyo kukamilika kwake kutakuwa ni fursa nzuri wa wafanyabiashara kukuza shughuli za kiuchumi. 

Daraja hilo  lina kimo cha meta saba (7) na upana wa meta kumi (10) njia za magari na meta tatu (3) njia ya waenda kwa miguu na ujenzi wake utakamilika Aprili 16 mwaka huu.

About the author

mzalendoeditor