Featured Kitaifa

WAZIRI MHAGAMA AWEKA WAZI MAFANIKIO YA WIZARA YAKE KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 16,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

Watumishi na Waandishi wa Habari wakifatikia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama leo March 16,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia.

……………………………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora,Jenista Mhagama ametaja mafanikio nane  ambayo Wizara hiyo imeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

UTAWALA BORA

Akitaja mafaniko hayo mbele ya Waandishi wa Habari leo Machi 16,2022 Jijini  Dodoma ,Waziri Mhagama amesema  Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia  katika kipindi cha mwaka mmoja imepata mafanikio makubwa katika eneo la utumishi wa umma na utawala bora.

Amesema mafanikio haya yanatokana na azma ya Rais ya kutaka kuujenga utumishi wa umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

MAGEUZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Waziri Mhagama amesema Serikali ya awamu ya sita imeweza kusimamia mageuzi katika utumishi wa Umma katika kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara.

“Rais alituelekeza kuwapandisha vyeo/madaraja Watumishi 190,781 wenye sifa

stahiki. Mhe. Rais aliamua tutumie jumla ya shilingi bilioni 39,649,988, 204 na kazi inaendelea.

Pia, Rais aliagiza yalipwe  madeni ya mishahara ya Watumishi wa

Umma 65,394 yenye thamani ya shilingi bilioni 91,087,826,006.34

“Kuwabadilisha kada Watumishi wa Umma 19,386 na kuwalipa mishahara mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 1,330,306,572.Kutoa vibali12,336 vya ajira mpya na mbadala ambapo jumla ya shilingi bilioni 7,761,869,809 zimelipwa.Kuwapunguzia kodi watumishi wa umma kutoka asilimia 9 mpaka 8,”amesema.

MFUMO MPYA PIPMIS 

Waziri Mhagama amesema wamefanikiwa kuangalia upya Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi (OPRAS) ili kupata mfumo sahihi wa usimamizi wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini pamoja nakuimarisha mifumo ya uwajibikaji.

Amesema mifumo hiyo  itahakikisha Viongozi na Watumishi wa Umma katika ngazi zote wanawajibika kwa hiari katika kufikia malengo waliyojiwekea katika taasisi zao.

Aidha, katika kipindi hiki Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi Public Institutions Performance Management Information System (PIPMIS).

“Mfumo huu ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Amesema Makubaliano hayo yatakuwa kati ya viongozi wakuu wa Taasisi na Viongozi wao wanaowasimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa kila siku.

“Malengo yaliyomo ndani ya mikataba yatakuwa na vigezo,shabaha na viashiria vitakavyotumika katika utendaji wa taasisi kila mwaka.

“Utekelezaji wa Mfumo wa Huu wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na taifa kwa ujumla; kuimarisha utamaduni unaojali matokeo; na kuleta matumizi bora ya rasilimali za umma,”amesema.

UJENZI WA MIFUMO YA TEHAMA

Amesema mafanikio mengine ni Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA inayohusu uendeshaji wa Serikali wa kila siku, kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma na kuimarisha maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwa kutumia mifumo.

Amesema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kujenga Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI kwa lengo la kuwawezesha watumishi na wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Waziri.

Aidha, mfumo huo unampa fursa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kufuatilia

namna masuala ya utumishi na Utawala Bora yaliyowasilishwa na wananchi na watumishi wa Umma yalivyofanyiwa kazi na kumuwezesha Waziri kufuatilia hali ya uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utumishi na utawala bora.

MAKAZI BORA

Amesema Wizara imeanza kutengeneza mfumo wa kuendesha mfuko wa revolving utakaosaidia ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu zitakazoweza kuwanufaisha wafanyakazi wa kada zote.

Vilevile, imetengeneza mpango kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutatua tatizo la makazi kwa watumishi kwa maeneo ya pembezoni.

Amesema katika kuwezesha watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kupata makazi bora na yenye gharama nafuu, Watumishi Housing inaendelea na ujenzi wa nyumba 80 katika eneo la Kisasa, Njedengwa jijini Dodoma.

SERA NA KANUNI

Pia,imeendelea  kuhuisha sera na kanuni za Utumishi wa Umma ili ziendane na mazingira na mahitaji ya sasa ya ujenzi wa uchumi na maendeleo ya taifa.

“Kujenga uwezo wa Viongozi na Watumishi wa Umma ili waweze kuwatumikia wananchi kikamilifu.

MALALAMIKO

Amesema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kupitia Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kuhakikisha haki inatendeka kwa Watumishi wa Umma wenye malalamiko dhidi ya waajiri wao.

Amesema katika kipindi hiki imeshughulikia na kutolea uamuzi rufaa 313 na malalamiko 174 ya watumishi waliochukuliwa hatua na mamlaka zao za nidhamu.

UTAFITI WA CPI NA RUSHWA

Waziri Mhagama amesema Ofisi ya Rais Utawala Bora kupitia TAKUKURU na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imefanikiwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla pamoja na kuimarisha maadili ya viongozi.

Amesema Taarifa ya utafiti iliyofanywa na Transparency International ya mwaka 2021 katika kiashiria cha Corruption Perception Index (CPI) kinaonesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika masuala ya rushwa.

Amesema imeweza  kufanya vizuri kwa kupata alama 39 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180, ikiwa imepanda kwa nafasi 7 ikilinganishwa na nafasi ya 94 ya mwaka 2020. Nchi yetu imeshika nafasi ya pili kwa Ukanda.

TASAF

Waziri huyo amesema Ofisi ya Rais Utawala Bora kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) imeendeleza juhudi za kupambana na umaskini na kuimarisha uchumi wa kaya maskini kupitia

miradi mbalimbali.

Amesema wameweza kukamilisha utambuzi na uandikishaji wa kaya ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa Kipindi cha Kwanza cha Mpango.

“Jumla ya Kaya 602,672 zimetambuliwa kutoka katika vijiji 7,217 ambapo kati ya hizo, kaya 494,348 (82.0%) zimekidhi vigezo vya umaskini na kuingizwa kwenye Mpango,”amesema.

Amesema Kaya hizi pia zimepokea ruzuku kwa mara ya kwanza mwezi Januari 2022.

About the author

mzalendoeditor