Featured Kitaifa

‘TANZANIA INATAMBUA UMUHIMU WA USHIRIKI WA WANAWAKE KULETA MATOKEO CHANYA KWA JAMII’: WAZIRI GWAJIMA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akiwasilisha taarifa ya nchi katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano wa mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani unaofanyika jijini New York nchini Marekani.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano wa mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani unaofanyika jijini New York nchini Marekani.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akifuatilia mawasilisho kutoka mataifa mbalimbali katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano wa mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani unaofanyika jijini New York nchini Marekani kushoto ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Mwajuma Magwiza.

…………………………………………………..

Na WMJJWM- New York Marekani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake kuanzia ngazi ya chini kwenye jamii ambayo itawezesha kupata matokeo chanya yatakayotoa majibu na tija kwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, mazingira na majanga kwa kuzingatia usawa wa jinsia.  

Dkt Gwajima ameyasema hayo Machi 15 jijini New York nchini Marekani katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano  wa 66 wa hali ya wanawake duniani.

Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye juhudi za kutunza mazingira, kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na majanga na kwa sababu hiyo imesaini makubaliano mbalimbali ikiwemo azimio la Beijing, azimio la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa(UNFCC), Azimio la Kyoto 1997, Ajenda 2030 na CEDAW.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa kinara wa utekelezaji wa jukwaa la kizazi chenye usawa kwenye eneo la uwezeshaji wa haki za kiuchumi, eneo linalolenga kuwezesha uhakika wa upatikanaji wa chakula, uchumi na maisha bora kwa ujumla. 

 Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja wanatekeleza Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia na kwa pamoja wameandaa Sera ya Taifa ya Mazingira inayotekelezwa kwa ushirikiano na wadau ili kuwezesha jamii zilizo kwenye athari zaidi.

Akihitimisha taarifa yake Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa, Tanzania itafanya Sensa ya watu na makazi kwa Mwaka huu wa 2022 Ifikapo Mwezi Agosti ambayo Shabaha yake ni kutoa picha ya wakati wa sasa kuhusu hali ya hewa na mazingira kwa ujumla wake.

Amesema kuwa baada ya kutolewa taarifa hiyo itasaidia wadau mbalimbali kushirikiana na Tanzania katika kufikia malengo ya kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira kwa kuja na sera, mipango na mikakati mizuri zaidi.

Waziri Dkt. Gwajima ameongoza ujumbe wa Tanzania New York nchini Marekani kushiriki mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani uliojumuisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Mwajuma Magwiza, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia Badru Abdulnoor na Maafisa wengine wa Wizara.   

 Mkutano wa wa 66 wa hali ya wanawake duniani umeanza Machi 14, 2022 na utaendelea hadi Machi 24, 2022 ambapo pamoja na mambo mengine utaangalia usawa wa jinsia katika sera, mipango na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, mazingira na majanga mbalimbali. 

About the author

mzalendoeditor