Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitawalishwa kuwa kiongozi wa wazee wa Mkoa wa Manyara kwa jina Akoo kutoka kwa wazee wa mila wa kabila la Gorowa leo tarehe 16 Machi 2022 wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa dini na wazee wa mkoa wa Manyara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na wazee pamoja na viongozi wa dini wa Mkoa wa Manyara katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria kilichopo Babati leo tarehe 16 Machi 2022 alipohitimisha ziara yake mkoani humo.

*************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 16 Machi 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi  pamoja na Viongozi wa Dini wa Mkoa wa Manyara, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Babati mkoani Manyara.

Akisoma risala kwa niaba ya wazee wa mkoa wa Manyara katibu wa Wazee Naomi Kapambala amesema wanafurahishwa na mwenendo wa serikali ya awamu ya sita katika kutatua kero mbalimbali pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha ameiomba serikali kukamilisha kujengwa kwa vitengo  vyote katika hospitali ya Rufaa ya mkoa pamoja na kuwekwa vifaa tiba ili kupunguza gharama za wananchi wakiwemo wazee kwenda mikoa ya jirani ya Dodoma na Kilimanjaro kufuata huduma za matibabu. Pia Bi. Naomi ameomba kutatuliwa kwa mgogoro wa mpaka uliopo baina ya hifadhi ya taifa ya Tarangire na vijiji vya Gijadabung,ayamango na Gedamar Wilaya ya Babati Vijijini.

Akizungumza na wazee hao pamoja na viongozi wa dini, Makamu wa Rais amewaasa kuendelea kuliombea taifa na wakati wote kutoa ushauri utakaoongza taifa katika amani na mshikamano. Makamu wa Rais amesema baraza ya wazee yanapaswa kutumika ipasavyo mkoani Manyara ili kuendelea kulinda maadili ya chama pamoja na jamii. Amesema wazee wanapaswa kuendeleza mila na desturi za watanzania ili kuwasaidia vijana kuwa wazalendo kwa nchi pamoja na tabia njema.

Halikadhalika, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wazee husasani katika sekta ya afya na mafao. Amewasisitiza watendaji waliopo katika mifuko ya mafao pamoja na hazina kuongeza kasi ya ulipaji wazee mafao yao kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Trioni 1.2 kwaajili ya ulipaji mafao.

Katika mkutano huo, wazee wa mila wa kabila la Gorowa wamempa uongozi wa kabila hilo kwa jina la Akoo pamoja na uongozi wa wazee wa mkoa wa Manyara Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.

Previous articleKAMATI YA SIASA CCM  MKOA WA ARUSHA WAMSHUKURU RAIS SAMIA, AMEWAPA MKURUGENZI ANAYEJALI MASLAHI YA WANANCHI.
Next articleTANGA UWASA YATUMIA BILIONI 22.2 UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI KATIKA KIPINDI CHA AWAMU YA SITA INAYOONGOZWA NA RAIS SAMIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here