Tukio hilo limetokea usiku wa kumkia leo, ambalo limeguduliwa majira ya saa 12 alfajiri na waokota uchafu kufika kwenye Ghuba hilo, na kuanza kutafuta mali mbalimbali ndipo walipofunua mfuko mmoja wakijua huenda kunavitu vizuri na kukuta vichanga hivyo ambavyo ni mapacha vikiwa tayari vimefariki.
Mmoja wa majirani wa eneo hilo la kuhifadhia uchafu Costantine Samweli, alisema mara baada ya waokota uchafu kuona vichanga hivyo vimekufa, ndipo wakaanza kupiga kelele na wao wakatoka kushuhudia tukio hilo na kuvikuta ndani ya mfuko vikiwa vimeshafariki.
“Ukiviangalia vizuri vichanga hivi huyu mama alivitoa vikiwa bado havijafikisha miezi Tisa, sababu hapa pembeni kama unavyoona kuna Sindano na baadhi ya vitu ambavyo vimetumika kumtolea watoto hawa,”alisema Samweli.
Nao baadhi ya akina mama ambao walifika eneo hilo la tukio, kwa nyakati tofauti walilaana kitendo hicho huku wengine wakiangua kilio, na kuiomba Serikali imtafute mwanamke ambaye amefanya unyama huo, na wamchukulie hatua kali za kisheria na liwefundisho kwa wengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Majengo Majid Issa, alisema tukio kama hilo la kutupa vitoto vichanga katika ghuba hilo la uchafu ni la pili, na kutoa wito kwa wanawake kama mimba zao au watoto wanakataliwa na wanaume wasiwafanyie ukatili, bali wawapeleke kwenye vituo vya malezi ya watoto.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kubainisha wanafanya uchunguzi ili kumbaini mwanamke aliyefanya unyama huo.