Kijana mmoja ameshtakiwa katika Mahakama ya Milimani nchini Kenya kwa kosa la kumshambulia mdogo wake kwa kumfinya sehemu zake za siri na kumsababishia madhara ya mwili.
Collins Cheruyot anadaiwa kumvamia mdogo wake, Allan Sang wakiwa katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi baada ya kutuhumiwa kuiba simu na pesa zake.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyosomwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa Serikali James Gachoka, Sang aliripoti polisi kwamba kaka’ke Collins aliiba simu yake ya Ksh 9,399 na kitambulisho chake.
Inasemekana Collins tayari alitumia simu hiyo ya mdogo wake kukopa fedha kiasi cha Ksh 12,316 kupitia huduma ya Mshwari kwa kutumia simu hiyo.
Baada ya mdogo wake kugundua kuwa kaka yake amemfanyia umafia huo, aliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Capital Hill , baada ya mtuhumiwa kusikia kuwa ameshtakiwa Polisi, alimvamia mdogo mtu kwa kumuumiza sehemu zake za siri na kumng’ata kidole.
Hakimu Mwandamizi Bernard Ochoi hata hivyo alilazimika kuahirisha hukumu ya mshtakiwa baada ya kuugua kortini ghafla na kuamuru apelekwe hospitali kwa matibabu. Kesi hiyo itatajwa Februari 24, 2022.