Featured Kitaifa

WAZIRI NDALICHAKO AWEKA WAZI MAFANIKIO YA WIZARA YAKE KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 13,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi ,Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Prof.Joyce Ndalichako,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa  waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 13,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

Watumishi na Waandishi wa Habari wakifatikia hotuba ya Waziri  wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Prof.Joyce Ndalichako (hayupo pichani),leo March 13,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia

……………………………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi  ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Wenye Ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako ametaja mafaniko 10 ambayo Wizara yake imeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mafanikio hayo ni katika kukuza ujuzi nchini,kazi na wafanyakazi,uwekezaji,utatuzi wa migogoro kazini,OSHA  kuongeza kaguzi,kutoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu, kuboresha mafao ya fidia kwa wafanyakazi,kulipa mafao kwa wakati, kushughulikia masuala ya vijana na Wastaafu kulipwa zaidi yay a shilingi trilioni 1.15

UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA KUKUZA UJUZI NCHINI

Akizungumza leo March 13,2022 jijini Dodoma na waandishi wa Habari kuhusu mafanikio hayo katika Wizara yake, Waziri Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kujenga ujuzi kwa watanzania ili kuhakikisha wanashiriki kwa ufanisi zaidi katika shughuli za uzalishaji mali sambamba na kuongeza fursa za ajira.

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini kwa kufanya kuongeza wigo wa fursa za mafuzo kwa vijana kutoka vijana 10,113 kwa kipindi cha mwaka mmoja kilichoishia Machi, 2021 hadi vijana 22,899 kwa kipindi cha mwaka mmoja kilichoishia Machi, 2022.

Aidha, wigo wa utoaji wa mafunzo umeongezeka kutoka vituo 17 katika Mikoa 13 hadi vituo 72 katika Mikoa 26.

Pia,kuwezesha Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi (Internship) kwa wahitimu 2,215 wa Elimu ya Juu na ya Kati kupitia waajiri wa sekta binafsi na sekta ya umma.

Vilevile,kutoa Mafunzo ya kurasimisha ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi kwa Watanzania 2,644 ambapo kati ya0 2,537 mawefaulu na kupata vyeti vya VETA.

“Kuendelea na mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa njia ya Uanagenzi kwa vijana 14,440.Tumejenga Viatalu Nyumba (Greenhouse) katika Halmashauri 36 za Mikoa mitano ya Arusha, Dar es Salaam, Pwani, Tabora na Singida.

“Sambamba na ujenzi wa Vitalu nyumba, vijana 720 wamwpatiwa mafunzo ya ufundi wa kujenga vitalu nyumba,”amesema.

Aidha, mafunzo ya namna ya kulima kwa kutumia vitalu nyumba yanaendelea kutolewa kwa vijana 3,600 (100 kutoka kila Halmashauri).

Amesema Idadi hiyo inafanya kuwa jumla ya vijana 12,850 kutoka Halmashauri 117 na Mikoa 17 ambao wamepatiwa mafunzo hayo.

MASUALA YA KAZI NA WAFANYAKAZI NCHINI

Waziri Ndalichako Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuhakikisha mazingira ya kazi na haki za wafanyakazi nchini yanasimamiwa ipasavyo kwa, kuimarisha taasisi za kazi nchini.

Pia, kuboresha vyombo vya utoaji haki mahala pa kazi, na kuwezesha upatikanaji wa haraka wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni.

KUIMARISHA UWEKEZAJI NCHINI

Katika kuhakikisha wanaimarisha  mazingira ya uwekezaji nchini, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu  Aprili 6 2021 alielekeza kuimarishwa kwa mfumo wa utoaji vibali vya kazi kwa raia wa kigeni.

“Hivyo, Ofisi ilifanikiwa kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji wa Vibali vya Kazi kwa Wageni na kuanza kutumika tangu tarehe 28 Aprili, 2021.

“Mfumo huu umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali kutoka siku za kazi 14 hadi siku 7 kutokana na kupungua kwa hatua za uombaji na uchakataji wa kibali kutoka hatua 33 hadi hatua 7.

“Mfumo umeimarisha uwazi na uwajibikaji na kupunguza vihatarishi vya rushwa katika kushughulikia vibali,”amesema.

Pia, katika kipindi cha mwaka mmoja cha Uongozi, Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imefanya mabadiliko ya viwango vya riba vilivyokuwa vikitozwa kwa waajiri waliokuwa wakichelewa kulipa michango kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoka asilimia 10 kwa mwezi hadi kufikia asilimia 2 kwa mwezi.

Amesema lengo la hatua hii ni kupunguza malalamiko ya muda mrefu ya waajiri na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Aidha, Serikali imepunguza mchango wa waajiri wa Sekta Binafsi katika kuchangia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoka asilimia moja (1%) hadi asilimia sifuri nukta sita (0.6%).

UTATUZI WA MIGOGORO KIKAZI

katika kushughulikia utatuzi wa migogoro ya kikazi nchini, kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA), umewekwa mfumo madhubuti wa kielektroniki wa kusajili na kushughulikia migogoro ya kikazi ambao umewezesha migogoro ya kikazi kutatuliwa kwa wakati, uwazi, kirafiki na kwa gharama nafuu.

Amesema muda wa kushughulikia mgogoro umepungua kutoka siku 30 hadi 14 katika hatua ya usuluhishi, na katika hatua ya uamuzi muda wa kushughulikia umepungua kutoka miezi sita hadi miezi mitatu.

Amesema kutokana na mfumo huo, Tume imefanikiwa kumaliza mashauri 13,115 kati ya mashauri 16,600 ndani ya mwaka mmoja ambapo kabla ya mfumo huo mashauri yasiyozidi 8,000 ndiyo yalikuwa yanashughulikiwa kwa mwaka.

Waziri Ndalichako amesema mashauri 3,485 yaliyobaki yameingizwa kwenye mfumo wa usikilizwaji wa mashauri kwa haraka (Crash Program) na yanategemewa kumalizika kwa wakati kwa mujibu wa Sheria.

“Hatua hii imeokoa ajira za wafanyakazi, imewezesha wafanyakazi kulipwa fidia, na kuweka msukumo kwa waajiri kufuata Sheria.

Pia imewezesha kupunguza kwa kiwango kikubwa migomo na viongozi kufungiwa nje ya ofisi.

Amesema kumalizika kwa mashauri kumeleta mazingira tulivu mahali pa kazi na kuwawezesha waajiri na waajiriwa kushiriki kwa ufanisi Zaidi katika uzalishaji wenye tija.

OSHA NA KAGUZI 96,693

Kuhusu Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa kazi (OSHA) ulishiriki na kushinda mashindano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa masuala ya usalama na afya sehemu za kazi na kuzishinda nchi nyingine kumi na sita (16) za Jumuiya ya SADC.

Aidha, katika kipindi cha mwaka mmoja taasisi ya OSHA imefanya kaguzi 96,693 za usalama kazini ikilinganishwa na kipindi kama hicho ambapo wakala ulifanya kaguzi chini ya 60,000.

Vile vile, upimaji afya umeongezeka kutoka Wafanyakazi 125,616 hadi kufikia Wafanyakazi 141,719 katika kipindi hicho.

Vilevile, kumekuwa na Ongezeko la mafunzo yaliyotolewa kuhusu Afya na Usalama Mahali pa Kazi, kutoka Wafanyakazi 3,144 hadi wafanyakazi 4,586 kwa mwaka.

KUTOKA SIKU 14 HADI MOJA

Amesema Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa kazi umeendelea kupunguza muda wa kupata cheti cha usajili wa sehemu za kazi kutoka siku 14 hadi siku 1 kwa kuweka mfumo wa kielektroniki (Online registration).

Pamoja na kupunguza muda wa kutoa Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi (Compliance License) kutoka siku 28 hadi siku 3.

HUDUMA NA MAFUNZO KWA WATU WENYE ULEMAVU

Katika kuimarisha Huduma na Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu nchini, Serikali imefanya ukarabati wa miundombinu iliyokuwa imechakaa katika Vyuo vya Watu Wenye Ulemavu.

Waziri Ndalichako amevitaja Vyuo hivyo ni Chuo cha Yombo – Dar es Salaam ambacho ukarabati wa mabweni umefanyika hivyo kuongeza udahili kutoka wanafunzi wenye Ulemavu 64 hadi 120

Chuo cha Masiwani, Jijini Tanga kimekarabatiwa miundombinu yake ikiwemo mabweni, nyumba za walimu, madarasa, Ofisi na uzio. Chuo hicho kitafunguliwa mwishoni mwa mwezi Machi, 2022 na kitadahili wanafunzi wenye ulemavu 96.

Chuo cha Luanzari, Tabora ambacho kilifungwa tangu mwaka 1997 kimefunguliwa tarehe 01 Agosti, 2021 ambapo kwa sasa kina wanafunzi 48 wenye ulemavu.

“Tumepokea shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa vyuo vitano vya Watu wenye Ulemavu nchini na taratibu za manunuzi zimekamilika.

Aidha Serikali imepanga kujenga vyuo vipya viwili (2) na kuendelea na ukarabati wa vyuo vitano (5) vya Watu wenye Ulemavu.

MAENDELEO YA VIJANA

Waziri Ndalichako amesema  ili kuimarisha uzalendo kwa vijana na Watanzania kwa ujumla, Serikali imeendelea kuratibu shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo pamoja na mambo mengine Mwenge wa Uhuru unahamasisha uanzishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii.

“Kwa mfano, mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zilizozinduliwa rasmi tarehe 17 Mei, 2021 kusini Unguja, Zanzibar na baadae kukimbizwa katika Wilaya 150 za kiutawala kwenye Mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania.

“Miradi ya maendeleo 1,067 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.2 ilizinduliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru.

“Miradi iliyofanyiwa kazi na Mwenge wa Uhuru iligusa Sekta ya Elimu, Maji, Afya, Mazingira, Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Barabara, Utawala bora, TEHAMA na Sekta ya Fedha,”amesema.    

Serikali imeendelea kuratibu na kusimamaia shughuli za maendeleo ya vijana kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imongeza mtaji wa Mfuko wa maendeleo ya vijana kutoka Shilingi bilioni 6.1 zilizokuwepo hadi kufikia shilingi bilioni 7.123.

Amesema katika kipindi hiki jumla ya shilingi bilioni 20.38 zimetolewa kupitia mifuko ya uwezeshaji vijana kwa vikundi vya vijana 4,035 vyenye vijana 45,373. “Fedha hizi ni mahususi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Aidha,Serikali imeandaa utaratibu maalum wa utoaji wa fedha hizo kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi, makampuni ya vijana na kijana Mmoja mmoja kupitia mwongozo mpya wa utoaji mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana.

“Nichukue nafasi hii kwa dhati kumshukuru mheshimiwa Rais kwa kuwapa kipaumbele vijana na kuhakikisha wanawezeshwa ili kuendeleza shughuli zao za uzalishajimali,”amesema.

KUIMARISHA HUDUMA ZA KINGA YA JAMII

Waziri Ndalichako amesema ili kuhakikisha huduma ya kinga ya Jamii nchini inaimarishwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa wigo wa wanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii unaongezeka kwa kujumuisha sekta isiyo rasmi.

Pia,Wastaafu wanalipwa Mafao yao kwa wakati na Wanachama wanapata elimu kuhusu hifadhi ya jamii.

WASTAAFU WALIPWA ZAIDI YA TRILIONI 1.15

Amesema katika kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais yaliyotolewa katika sherehe za Mei mosi mwaka 2021, ambapo alielekeza kuwa madai ya mafao ya wastaafu yaliyocheleweshwa yaanze kulipwa kuanzia mwezi Mei, 2021 na kuendelea kulipwa hadi mrundikano utakapokwisha.

Amesema  Mfuko umetekeleza maagizo hayo na umelipa Mafao yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.15 kwa wanufaika, yaani wastaafu na wategemezi wapatatao 51,079.

Vile vile Mfuko umelipa kiasi cha shilingi bilioni 692.38 ikiwa ni pensheni ya kila mwezi, kiasi ambacho ni sawa na wastani wa shilingi bilioni 57.70 kila mwezi kwa wa wastaafu 147,459 kwa mwezi.

Amesema kiasi hiki cha pesa hulipwa kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi husika bila kukosa.

Hadi kufikia mwezi Februari 2022 Mfuko umekamilisha kulipa madai yote ya muda mrefu.

Amesema katika kuongeza kasi ya ulipaji mafao kwa wastaafu, Serikali ya Awamu ya Sita, imelipa jumla ya shilingi Trilion 2.17 kupitia Hati Fungani.

Waziri huyo amesema fedha hiyo ni sehemu ya deni la shs Trilioni 4.6 iliyotumika kufanya malipo kwa wanachama waliostaafu ambao hawakuchangia katika kipindi cha kabla ya mwaka 1999.

Aidha, katika kipindi hicho Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 200 kati ya deni la shs 431 bilioni la mikopo ya Uwekezaji lililokuwepo wakati Serikali ya awamu ya 6 ilipoingia madarakani.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja Mfuko wa PSSSF umeweza kusajili wanachama wapya wapatao21,461 sawa na asilimia 116.74 ya lengo la kusajili wanachama wapya 18,384 kwa kipindi husika.

Amesema Wanachama hao  waliondikishwa kwa zaidi ya asilimia 60 wametokana na ajira mpya za kada za Afya na Walimu walioajiriwa na Serikali katika.

Amesema Katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata maslahi na haki zao za mafao, Mfuko wa NSSF umeongeza kasi ya kusajili wananchama.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko umeandikisha jumla ya wanachama wapya 185,288 sawa na ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na wanachama wapya 155,192 walioandikishwa katika kipindi cha mwaka mmoja ulioishia Februari, 2021.

Amesema kati ya wanachama hao, wanachama 153,119 waliandikishwa kutoka sekta rasmi na wanachama 32,169 waliandikishwa kutoka sekta isiyo rasmi.

Pia Mfuko uliandikisha waajiri wapya 1,605, hivyo kufanya idadi ya waajiri kufikia 34,049 sawa na ongezeko la asilimia 4.9.

Aidha, katika kipindi hicho, Mfuko umekusanya michango ya shilingi bilioni 1,129.4 sawa na ongezeko la asilimia 5 ya michango ya shilingi bilioni 1,075.3 iliyokusanya katika kipindi cha mwaka mmoja ulioishia Februari

2021.

Waziri Ndalichako amesema  katika kuboresha mafao ya fidia kwa wafanyakazi, Serikali imeongeza kiwango cha juu cha pensheni kutoka shilingi zaidi ya milioni 3.6  na kufikia zaidi ya  shilingi milioni  8  kwa mwezi.

Amesema ongezeko hilo, limekuwa faraja kubwa kwa wafanyakazi na waajiri nchini na linachangia kupunguza umaskini kwa wategemezi wa wafanyakazi wanaofariki kutokana na kazi.

About the author

mzalendoeditor