Featured Kitaifa

GSM ATOA VIELELEZO UMILIKI WA ARDHI,MAKONDA AMJIBU

Written by mzalendoeditor

Wakati Wakili wa mfanyabiashara maarufu nchini, Ghalib Said Mohamed (GSM), Alex Mgongolwa ameweka wazi vielelezo vya umiliki wa eneo kiwanja namba 60 lililopo Regent Estate Kinondoni jijini hapa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka mfanyabiashara huyo kumwachia mali yake.

Mzozo wa kiwanja hicho umeibuka hivi karibuni, ambapo Makonda ameonekana katika video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa eneo hilo ni lake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Machi 12, 2022 jijini hapa Wakili Mgongolwa amemtaka mtu ambaye hakumtaja kwa jina, kuweka wazi vielelezo alivyonavyo vya umiliki wa eneo hilo na vielelezo kutoka Wizara ya Ardhi vinavyompa uhalali wa kulimiliki.

Hata hivyo, Makonda alipotafutwa kwa simu leo, amejibu kwa ujumbe wa WhatsApp, akisema; “GSM usinilazimishe kusema uozo wako achia mali yangu. Walioko nyuma yako nawajua.”

Kama hiyo haitoshi, katika ukurasa wake wa Instagram, Makonda aliweka video ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ambayo pamoja na mengine alieleza haja ya kutaka Jeshi la Polisi kuchunguzwa, kisha akaweka ujumbe:

“Naunga mkono hoja ya Kamati Kuu, ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi, wanaolipaka tope Jeshi la Jolisi kwa kuwalinda wafanyabiashara MATAPELI wanaodhulumu mali za watu. Naomba tuanze na Dar es salaam na mimi Paul Makonda niko tayari kutoa ushirikianao.”

Akifafanua zaidi kuhusu umiliki wa ardhi hiyo, Wakili Mgongolwa amesema, mteja wake Ghalib Said Mohamed alinunua ardhi wilaya ya Kinondoni, eneo la Regent Estate plot no. 60, title no. 186153/60, kwa lengo la ujenzi wa makazi Novemba 21, 2006.”

Vilevile, Mgongolwa amesema Septemba 2017, mteja wake aliingia mkataba na kampuni ya ujenzi iitwayo Group Six International (Contract Class One) kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo wenye thamani ya Sh640 milioni.

“Ghalib aliomba kibali cha ujenzi na manispaa ya Kinondoni walitoa kibali hicho Oktoba 16, 2017 chenye kumbukumbu namba 00020032 kwa Ghalib Said Mohammed kwa ajili ya ujenzi eneo hilo,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kibali hicho kutoka, Group Six walianza ujenzi na walipeleka malipo ya awali ya ujenzi Januari 31, 2018 huku mteja wake huyo akitekeleza sehemu ya mkataba kwa kulipa kiasi cha Sh51.92 milioni, malipo ambayo yana kithibitisho kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kuhusu mteja wake kuwa na uhusiano wa karibu na mlalamikaji, alisema, “mteja wangu na mtu ambaye kwenye mitandao amekuwa akizungumza kwamba anamiliki eneo hilo, mteja wangu katika kipindi anachozungumza huyo mtu cha mwaka 2012 alikuwa hamfahamu kabisa huyo mtu.”

“Mimi leo nathibitisha uhalali wa miliki, unaweza ukawa na uhusiano na mtu lakini sio wa kibiashara wa kuuziana na kuhamishiana miliki licha ya kuingia katika makubaliano ya kuhamishiana miliki,”

Mgongolwa alisema kufahamiana na mtu ni jambo lingine na miliki ni jambo lingine, hivyo ushahidi wa vielelezo kisheria unakingwa na vielelezo hivyo, ambaye anasema ni eneo lake aweke wazi vielelezo vya kisheria.

“Tunatoa changamoto kwa mtu yoyote yule aje akinzane na vielelezo vyetu, huu ni ujenzi kwa mujibu wa mkataba na haujasimamiwa na mjomba au shangazi,” amesema Mgongolwa.

Alisema yeye yuko radhi kumsikiliza ili wakapambane, alisema kama kuna mtu anadhani anayo haki katika umiliki huo, lakini kwa sasa hawatafanya chochote na endapo ataendelea na matukio hayo hivyo basi ngazi za kisheria zitafuatwa.

“Hata tunaondokana na hisia tunaenda na uhalisia, yoyote yule anayesema aridhi ni ya kwake iwe kimahusiano au lah, aje na vielelezo kwetu, mtu mwenye dhana tofauti milango ya kimahakama iko wazi, ila kwa sasa hawatakwenda mahakamani,” amesema Mgongolwa na kuongeza kuwa wajibu wangu kama mwanasheria ni kuthibitisha umiliki halali kwa mteja wangu.

“Hatua tutakazozichukua kuanzia sasa itategemea na matukio ambayo yatafuata kwani ndiyo yatatupa mwongozo wa nini tukifanye, ikitokea hatua ya kwenda mahakamani tutakwenda, ikitokea kuangalia ngazi nyingine tutalipeleka kwa kuwa maelekezo yetu yako wazi tunatakiwa kulinda haki ya teja wetu sambamba na jina lake,” amesema.

About the author

mzalendoeditor