Featured Kitaifa

BASHUNGWA ATAKA WAKUU WA MIKOA KUJIFUNZA KWA MTAKA UJENZI WA SOKO LA MACHINGA

Written by mzalendoeditor
Baadhi ya Wakuu wa mikoa,makatibu tawala na Wakurugenzi wakiongozwa na Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa kukagua ujenzi wa mradi wa soko la Machinga Dodoma unaotarajiwa kukamilika Mwezi Mei mwaka huu.
Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kukagua ujenzi wa soko la machinga Dodoma,mradi ambao amesema utarudisha hadhi ya machinga Nchini.
Msanifu mshauri wa mradi wa soko la machinga Dodoma Dkt. Ibrahim Msuya akimuelekeza jambo Waziri Bashungwa katika eneo unapojengwa mradi wa soko hilo na kueleza kuwa linatarajia kubeba zaidi ya machinga 3000 mara litakapokamilika huku likiwa na vizimba vya aina 90 vitakavyotumika kwa biashara tofauti tofauti.

…………………………………………………….

Na Bolgas Odilo-DODOMA

WAKUU wa Mikoa yenye Halmashauri zenye hadhi ya Majiji wametakiwa kutumia mbinu inayotumika katika ujenzi wa Soko la Wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex) katika eneo la Bahi Road jijini Dodoma ili kuboresha zoezi la upangaji wa machinga kulingana na Mazingira ya maeneo yao.

Wito huo umetolewa Leo tarehe 12 Machi, 2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake na wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala, na Wakurugenzi wa mikoa yenye hadhi ya majiji kutembelea ujenzi wa eneo hilo.

Akizungumza na viongozi hao, Bashungwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametambua sekta ya machinga kuwa rasmi hivyo kwa sasa wanaenda na maono yake ya kuhakikisha wanajengewa mazingira rafiki kwa kazi zao.

“Hapo awali changamoto ya machinga haikuwa na suluhu kwa sababu tuliyokuwa tunatafanya kuzitatua hayakuwa na uhalisia, hivyo kwa soko letu hapa baada ya maelekezo ya Rais kuwajengea mazingira rafiki tukaamua kutokwenda nje ya nchi kuiga wenzetu wanavyofana tukathamini vya ndani kwa kwenda eneo la Mnadani Msalato jijini hapa ili kuona ni namna gani watafanya biashara zao.

Napongeza ubunifu uliofanyika kwenye soko hili la machinga na namna jiji lilivyotafsiri maono ya Rais kwa kubuni masuala haya hii ni fursa kwa viongozi wengine wa mikoa yenye hadhi ya majiji kama Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya kujifunza kwa gharama ndogo hapa hapa nchini,” amesema Bashungwa.

Amesema kuwa ingewezekana kwenda nje ya nchi kubuni kitu ambacho tunaweza kujifunza sisi wenyewe hivyo tunajivunia suala hili na wakuu wa mikoa, makatibu Tawala na wakurugenzi nimewaomba mje hapa ili kutafsiri kwa vitendo kwenye ngazi za mikoa maana yapo mambo makubwa tunaweza kufanya, hivyo tumieni matamko ya viongozi na maono yao kufanya haya,”

Waziri Bashungwa amewataka viongozi hao kupeleka elimu waliyojifunza kwenye soko hilo kwenye maeneo yao na kuhakikisha wanawashirikisha machinga kwenye ujenzi wa miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwenye mikoa yenye hadhi ya majiji nchini.

Kwa upande wake, Msanifu mshauri wa mradi huo, Dk Ibrahim Msuya amesema soko hilo litaweza kubeba machinga 3000 na vizimba vya aina 90 za biashara tofauti tofauti.

Amefafanua kuwa kwa sasa wanafanya usajili wa machinga kwa mfumo wa kidigitali kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya baadhi kujisajili mara mbili jambo ambalo lilileta taswira mbaya.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohamed Builders Limited, Taher Mustafa alimshukuru Rais Samia kwa historia aliyoipa kampuni hiyo kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya serikali huku akiahidi kutekeleza kwa wakati.

“Namshukuru Rais Samia na uongozi wa jiji la Dodoma na maeneo mengine kwa kutuamini kampuni yetu na namhakikishia kuwa tutamaliza mradi kwa muda uliopangwa na kwa viwango ili izidi kutuamini na kutupa miradi zaidi,”amesema

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alisema wamejifunza kupitia mradi huo na kuahidi kuwa kwenye maeneo yao watazingatia kuwa dhamira ya Rais kuwawekea mazingira rafiki machinga linazingatiwa.

“Tunaomba kufanyia marekebisho kwenye bajeti zetu ili kuweka mpango huu hususani kwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2022/23,”amesema Homera

Wakuu hao wa mikoa waliofanya ziara ya kujifunza kuhusu mradi wa ujenzi wa soko la Machinga -Open Market, unaotekelezwa na jiji la Dodoma ni pamoja na  Tanga ,songwe,Mwanza Moro,Arusha,Iringa na Mbeya ambao kwa pamoja wameeleza kuwa kwenye bajeti zao watahakikisha wanaelekeza kwenye maboresho ya maeneo ya machinga.

About the author

mzalendoeditor