Featured Kitaifa

SERIKALI YA WILAYA YA MJINI ZANZIBAR YAKANUSA BANDA LA VYUMBA VIWILI LILILOBOMOLEWA NA MANISPAA YA MJINI UNGUJA HALIKUWA KANISA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kukanusha taarifa za uchochezi zinazosambazwa mitandaoni kuwa Manispaa ya Mjini imevunja Kanisa huko Sebleni Mkoa wa Mjini Unguja.

Haruna Haji Mkaazi wa Sebleni akielezea kufurahishwa kwa zoezi la kuvunjwa Mabanda na nyumba zilizojengwa bila vibali katika maeneo hatarishi huko Sebleni Wilaya ya Mjini Unguja.

…………………………

Na Kijakazi Abdalla        Maelezo  11/03/2022.

Serikali ya Wilaya ya Mjini Zanzibar imesema Banda la vyumba viwili lililobomolewa na Manispaa ya Mjini Unguja halikuwa Kanisa kama taarifa  zinavyosambazwa katika mitandao ya kijamii nchini.

Banda hilo na mabanda mengine yaliyopakana yamevunjwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kuelekea kipindi cha mvua za masika.

Akizungumza na vyombo vya habari Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja Rashid Simai Msaraka amesema Mamlaka ya hali ya hewa nchini imeagiza kuchukuliwa kwa tahadhari juu ya Mvua za masika hivyo Wilaya yake imeamua kuvunja Nyumba na Mabanda yote yaliyojengwa bila kufuata sheria.

Amesema Banda hilo lililobomolewa na mabanda mengine yote yamejengwa bila kufuata sheria katika maeneo hatarishi jambo ambalo linaweza kusababisha maafa kipindi cha mafuriko.

“Ukweli ni kwamba Banda hilo ambalo tumelivunja na mabanda mengine yalijengwa bila kupata Kibali. Hapakuwa na Kanisa wala nyumba yoyoye iliyojengwa ikiwa na Kibali. Tumevunja na tutaendelea kuvunja mabanda na nyumba zote zilizojengwa maeneo hatarishi na pasina kupatiwa kibali cha ujenzi” alisisitiza Msaraka

Akifafanua zaidi Msaraka amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoheshimu dini tofauti na kutii haki ya kuabudu ya kila Mtu.

Ameongeza kuwa Zanzibar toka enzi yapo Makanisa na hakuna mtu anayeweza kuyagusa au kuyadhuru kwa vile yapo sehemu salama na yamefuata sharia zote.

“Mtu yeyote ana haki ya kuabudu kupitia nyumba yake ya Ibada iwe Msikiti, Kanisa, Hekalu, na utaratibu huo upo enzi na enzi hapa Zanzibar” Amesema Msaraka.

Msaraka ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi Wilaya kuwakamata kwa mahojiano wale wote wanaosambaza taarifa za uchochezi zinazotia uvunjifu wa amani nchini.

About the author

mzalendoeditor