Featured Michezo

MSEMAJI WA SIMBA AHMED ALLY:’YANGA YA MAYELE INATISHA’

Written by mzalendoeditor

MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amekiri kuwa, watani wao wa jadi, Yanga SC, msimu huu wana kikosi bora tofauti na misimu iliyopita.

Yanga wanaongoza Ligi Kuu Bara wakiwa na alama 45, safu yake ya ushambuliaji inaongozwa na Fiston Mayele raia wa DR Congo akiwa amefumania nyavu mara 10.

Katika msimamo huo wa Ligi Kuu Bara, Simba wameachwa kwa tofauti ya  alama nane wakiwa na alama 37 huku kila timu ikiwa imecheza Timu zote mechi 17.

Akizungumza jijini Dar, Ally alisema Yanga msimu huu wamechachamaa na kuonesha nia ya wazi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao waliukosa kwa kwa miaka minne.

Ally alisema licha ya kuchachamaa huko kwa Yanga, lakini wao hawatishiki, kikubwa wanawapa tahadhari na umakini mkubwa katika mbio hizo za ubingwa.

“Lipo wazi kabisa, wapinzani wetu Yanga wana timu bora tofauti na misimu iliyopita na hiyo imetokana na usajili ambao wameufanya.

“Licha ya ubora wao huo, lakini hawatutishi kabisa katika mbio za ubingwa, kikubwa wao wanatupa tahadhari na umakini katika mbio hizi za ubingwa.

“Sisi pia tuna kikosi imara tulichokijenga kwa misimu minne ambacho leo kinaitangaza nchi kimataifa ambacho pia kitatupa ubingwa wa ligi kwa mara tano mfululizo,” alisema Ally.

Simba ndani ya misimu minne mfululizo sasa, imefanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, huku ikichukua Kombe la Shirikisho la Azam Sports mara mbili mfululizo.

About the author

mzalendoeditor