Featured Kitaifa

MBUNGE WA HAI ATANGAZA KUMALIZA CHUKI NA MWENYEKITI WA CHADEMA

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Hai mkoani Kilimanjaro, Saashisha Mafuwe (CCM), amesema yeye si muumini wa siasa za uadui, chuki na kuumizana, ndio maana alidiriki kumkaribisha nyumbani, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

Mafuwe alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Narumu katika mfululizo wa ziara zake jimboni humo. Machi 4, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), aliwasilisha mahakamani hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa ikimkabili Mbowe na wenzake watatu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Akizungumza na wananchi wa Narumu, Mbunge huyo alisema: “Acheni kuumizana kwa sababu ya siasa, acheni kuchukiana kwa ajili ya siasa, mmeona kilichotokea, baada ya Freeman Mbowe kuachiwa alienda wapi. Alienda kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

“Na mimi alivyotoka (Mbowe), si niliandika nikamwambia karibu nyumbani kaka; huo ndio undugu, hatutaki siasa za uadui za kuumizana. “Halafu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, anaenda kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa wanazungumza, mbunge anaenda kwa aliyekuwa mbunge, simnasikia misiba yote ya kwa Mbowe naendaga?

Kukiwa na sherehe mimi niko naye, halafu wewe unayegombana unagombana nini mzee! Utabaki peke yako, nakwambia mzee tafuta hela (pesa), utabaki peke yako.”

Aliongeza: “Sisi tunaelewana tukimaliza kampeni tunakaa wote tunakunywa soda, tunakunywa kahawa yetu. Nyie kununiana, acheni hiyo biashara. Siasa nzuri ndio hii tunayofanya ya maji, umeme, kilimo, hiyo ndiyo siasa, sio maneno na ugomvi ugomvi.

“Mnakuja kuumizana wenyewe kwa wenyewe hapa, halafu sisi baadaye tunaelewana, tunawaacha na majeraha. Tuache hayo mambo, watu wa Narumu nawapenda sana, nawaombeni tufanye siasa za kistaarabu na siasa zilishaisha sasa ni muda wa kazi.”

Aidha, Mbunge huyo aliisema, “Lakini kuna kitu mmejifunza, si ndio hiki mmejifunza hapa, wale ambao mlikuwa mnapambana, sisi tumeshaelewana huko, mtajua wenyewe. Cha kuambiwa changanya na cha kwako, pambana na tumbo lako, pambana na nyumba yako, tukija tukiwaeleza maneno tupeni tukafanye kazi.”

“Mmenituma mmeona kazi ninayoifanya, na sasa hivi naanza vijiji mpaka nitoboe vitongoji vyote viingine kwenye Hansad (kumbukumbu rasmi) za Bunge.

Keshokutwa mtasikia tela, ntataja vyote hicho ndicho mlichonituma na ndio siasa hiyo. Nadhani mmeona na ninyi Mbunge wenu siingii kwenye maugomvi ya watu au mmeshasikia nazungumza mambo ya kitaifa, naongea mlichonituma mimi, maji, barabara, umeme.

“Sasa na ninyi si muige, kwa nini mlete mambo ya chuki chuki. Kwa nini mnaumizana wenyewe kwa wenyewe. Halafu mnaumizana ili wewe uwe nani?

Akionya kuhusu vitendo hivyo, Mafuwe alisema kama mbunge hana chuki na mtu, Mwenyekiti wa Taifa, hana chuki na mtu, wewe hiyo chuki unaitoa wapi? Ndugu zanguni niwaombe tupendane, tushirikiane.

CHANZO:GLOBAL

About the author

mzalendoeditor