Na Angela Msimbira MVOMERO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua za kiutumishi wakuu wa Idara wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za Manunuzi kwenye ujenzi wa shule ya Sokoine Memorial High School, Mkoani Morogoro
Akiongea na uongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Leo tarehe 10 Machi, 2022 wakati akikagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo Waziri Bashungwa amesema kumekuwa na dosari kwenye Manunuzi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero lakini kumekuwa na dosari katika suala zima la manunuzi inayosababisha miradi kukwama na kutomalizika kwa wakati.
Ameendelea kufafanua kuwa kumekuwa na Dosari kwenye kunukuu bei kabla ya kupatiwa idhini na Mkurugenzi wa Halmashauri ambapo bei inatolewa alafu idhini inafuata baadaye jambo ambalo halikubaliki katika sheria za manunuzi
Bashungwa amesema kuwa dosari nyingine kuleta kwa mzigo kwanza ndipo local purchasing order inasiniwa ambapo ni kinyume na utaratibu pia utumiaji wa fomu za vivuli badala ya fomu halisi.
Ameendelea kufafanua kuwa dosari nyingine kwa upande wa Manunuzi ni kuwa upo ushahidi inaonyesha uteuzi wa wazabuni kupewa kazi wakati hawaKujaza fomu wakati wa kutafuta mzabuni, hivyo kuonyesha kuwa kuna udanganyifu upande wa Manunuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Aidha, amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kufuata sheria kanuni na taratibu za manunuzi katika kuendesha Halmashauri ili wasiingie kwenye matatizo ambayo yanatokana na kwenda kinyume na utaratibu.