Featured Kitaifa

SILINDE AZITAKA HALMASHAURI AMBAZO HAZIJAKAMILISHA UJENZI WA SHULE ZA KATA KUTOA TAARIFA

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Elimu) Mhe. David Silinde ameziagiza Halmashauri zote nchini zinazojenga shule mpya za kata zifuatilie maendeleo ya ujenzi na zihakikishe zinatuma taarifa sahihi Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Mhe. Silinde ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya Kata ya Masandaka Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro na kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi unaoendelea katika shule hiyo.

Amesema, hakuna sababu ya ujenzi huo katika shule hiyo mpaka sasa kuwa katika hatua ya msingi ikiwa Serikali imetoa fedha siku moja kwa shule zote na Halmashauri ya Moshi Vijijini wapo katika hatua ya uwezekaji.

“Natoa maelekezo ifikapo tarehe 15 Mei, 2022 shule hii iwe imekamilika na ujenzi wa shule uendane na thamani ya fedha zilizotolewa.

“Aidha, nazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kuisimamia fedha za miradi zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule ili kuhakikisha inakuwa na thamani ya fedha na hata watumiaji wanakuwa na imani ya samani unazozitumia,”amefafanua Mhe.Silinde.

Katika hatua nyingine, Mhe. Silinde alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Uru Kusini na kutokuridhishwa na ujenzi wa majengo ya zahanati hiyo ambayo walishapokea fedha zinazotokana na tozo za miamala ya simu shilingi milioni 250 toka miezi mitatu iliyopita, lakini bado maendeleo ya ujenzi huo hauridhishi.

“Sijaridhishwa na mwenendo wa kasi ya ujenzi unaojengwa, ninawaelekeza mkamilishe ujenzi huu kama ambavyo Serikali ilishawaelekeza hakuna sababu ya kutokuendelea kwa ujenzi wakati Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ilishatoa fedha” ameagiza Mhe.Silinde.

Amesema, fedha hizo zimetokana na kodi inayokusanywa kutoka katika fedha za tozo ya miamala, hivyo wananchi wanataka kuona thamani halisi ya fedha wanazokatwa zinafanyiwa kazi kwa maendeleo yao na waweze kupata huduma kwa haraka.

Amesema, ujenzi wa kituo hicho kikikamilika kwa haraka kitasaidia wananchi kupata huduma na kutotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi ameishukuru Serikali kwa kuwajengea kituo hicho cha afya na kuiomba Ofisi ya Rais- TAMISEMI kusimamia kukamilika kwa haraka ujenzi wa kituo hicho ili kuokoa maisha ya wananchi kutotembea umbali mrefu kufuata huduma.

About the author

mzalendoeditor