Featured Kitaifa

WATU SITA MBARONI KWA KUSAFIRISHA VIPODOZI NA KUKWEPA KULIPIA USHURU WA FORODHA

Written by mzalendoeditor

 

SITA WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA KUSAFIRISHA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU NCHINI NA KUKWEPA KULIPIA USHURU WA FORODHA. 

KUPATIKANA NA BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU KUINGIA NCHINI NA ZILIZOKWEPA KULIPIWA USHURU WA FORODHA.

Mnamo tarehe 06.03.2022 majira ya saa 18:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Mtaa wa Mwanyanje – Uyole, Kata ya Uyole, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya na kufanikiwa kumkamata ABDUL MWAKALINGA [27] Dereva Tax, Mkazi wa Uyole akiwa na bidhaa zilizozuiliwa kuingizwa nchini na zilizokwepa kulipiwa ushuru wa forodha kutoka nchini Zambia ambazo ni:-

  1. Vitenge jora 87,
  2. Nyavu za kuvulia Samaki matundu madogo viroba 10,
  3. Boksi 06 zenye vipodozi vyenye viambata sumu aina ya maji ya citrolight, Ct + Clear therapy, Cocoplus, Miss mimi
  4. Kiroba 01 chenye vipodozi aina ya Anti Blacks Spots, Stretch Marks and Pimples.
  5. Kiroba 01 chenye vipodozi aina ya Epiderm Crème.

Jumla ya mali yote iliyokamatwa ni zaidi ya milioni tisa. Mtuhumiwa ni msafirishaji na muuzaji wa bidhaa hizo zilizopigwa marufuku nchini na zilizokwepa kulipiwa ushuru wa forodha. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika. 

KUPATIKANA NA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU NCHINI. 

Mnamo tarehe 06.03.2022 majira ya saa 02:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kata ya Chimala, Tarafa ya Ilongo Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya na katika msako huo alikamatwa mtuhumiwa EMANUEL MSIGALA [42] Mkazi wa Uyole – Mbeya akiwa amepakia na kusafirisha vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini aina ya Coco Pulp kopo 90 kwenye Gari yenye namba za usajili T.512 DCS aina ya Toyota Hilux Surf. Mtuhumiwa ni mnunuzi, msafirishaji na muuzaji wa bidhaa hizo.

WITO WA KAMANDA: Ninatoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kufanya biashara halali na kuacha kukwepa kulipa ushuru kwa bidhaa wanazonunua nje ya nchi vinginevyo watafilisika kwani Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama, hakuna mwanya wa kupitisha bidhaa za magendo. Aidha ninatoa rai kwa wale wanaoendelea kuingiza na kusafirisha vipodozi vyenye viambata sumu na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini kuacha mara moja vinginevyo mkono wa serikali hautowaacha salama.

WATATU WASHIKILIWA KWA MAHOJIANO KWA KUMSHAMBULIA KIJANA MMOJA.

Mnamo tarehe 03.03.2022 majira ya saa 08:00 asubuhi huko Mtaa wa Igodima, Kata ya Iganzo, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya, Kijana aitwaye SHADRACK ZACHARIA [28] Mpiga Picha na Mkazi wa Igodima Jijini Mbeya anayeonekana kwenye “clip” ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii alishambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na viongozi wa kata ya iganzo kwa kile kinachoelezwa ni kutoa lugha ya matusi na kuwapiga picha bila idhini yao wakati wakifanya shughuli za maendeleo katika Mtaa wa Igodima.

Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na kukataa kutoa eneo kwa ajili ya kupitisha njia ya mtaa.

Awali mama wa mhanga aitwaye ESTHER ANDREW [58] Mratibu Elimu Kata na Mkazi wa Igodima kabla ya kununua eneo hilo wakazi wa eneo hilo walikuwa wanapita njia lakini baada ya kununua na kujenga nyumba aliziba njia ndipo wakazi wa mtaa huo walifika ofisi za kata kutoa malalamiko ambayo yaliamuliwa kwenye kikao kuwa kila upande utoe hatua moja ili kupitisha njia ya mtaa. Hivyo siku hiyo ya tarehe 03.03.2022 asubuhi Diwani wa Kata akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Mtaa na wananchi walifika hadi eneo husika na kuanza kuchonga barabara ndipo ugomvi ulitokea.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watuhumiwa watatu kwa mahojiano ambao ni:-

  1. DANIEL WILLIAM [35] Diwani wa Kata ya Iganzo.
  2. ERASTO MWANKENJA [48] Afisa Mtendaji Kata ya Iganzo.
  3. HENJE MBOMBO [74] Mkazi wa Iganzo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linalaani tukio hilo na linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watafute suluhisho la migogoro yao kwa kufuata njia zilizo sahihi ikiwa ni pamoja na kuvihusisha vyombo vya haki likiwemo Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutofuata sheria.

About the author

mzalendoeditor