Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI JUKWAA LA UCHUMI DUNIANI

Written by mzalendoeditor

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 8 Machi akishiriki Jukwaa la Uchumi la Duniani kwa Kanda ya Afrika lililofanyika kwa njia ya mtandao. Makamu wa Rais amekuwa mgeni rasmi katika majadiliano hayo yalioshirikisha viongozi mbalimbali wa serikali ,sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kutoka nchi za ukanda wa Afrika katika mada iliojadili namna teknolojia inavyoweza kutumika  katika kukuza biashara ndogondogo na za kati ili kuchangia uchumi kwa nchi za Afrika baada ya athari za Uviko 19.

*************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 8 Machi ameshiriki Jukwaa la Uchumi la Duniani kwa Kanda ya Afrika lililofanyika kwa njia ya mtandao. Makamu wa Rais amekuwa mgeni rasmi katika majadiliano hayo yalioshirikisha viongozi mbalimbali wa serikali ,sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kutoka nchi za ukanda wa Afrika katika mada iliojadili namna teknolojia inavyoweza kutumika  katika kukuza biashara ndogondogo na za kati ili kuchangia uchumi kwa nchi za Afrika baada ya athari za Uviko 19.

Akifungua Jukwaa hilo, Makamu wa Rais ametaja juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha uchumi na kuendeleza biashara ndogo ndogo na za kati kufuatia athari za Uviko 19 ikiwemo kupunguza na kuondoa baadhi ya kodi ili kunusuru biashara zilizokuwa zimeathiriwa na Uviko19. Aidha amesema serikali imewekeza katika kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuongeza ushirikiano na mataifa mbalimbali na kufungua biashara zilizokwama na kuathiriwa na Uviko19 pamoja na kuwavutia wawekezaji wa nje hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema serikali imekua ikiongoza majadiliano katika baraza la biashara ili kupata changamoto zinazowakumba wawekezaji na kuzipatia ufumbuzi wa haraka. Ameongeza kwamba ili kuinua uchumi serikali inatekeleza miradi mikubwa kama vile ya miundombinu,nishati na maji pamoja  na mingineyo ikiwemo ya tehama ili kuongeza ufanisi katika biashara na uwekezaji.

Aidha amesema kupitia kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko19 serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya, elimu, maji pamoja na kuinua biashara ndogo ndogo na za kati.

Makamu wa Rais amesema kupitia jitihada hizo tayari viashiria vya ukuaji uchumi vimeanza kuonekana pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji nchini, kuongezeka kwa watalii pamoja na uwekezaji katika sekta ya madini.

Amesema asilimia 90 ya biashara nchini Tanzania ni zile ndogo na za kati zinazochangia ajira kwa vijana na wanawake hivyo mpango wa taifa wa miaka mitano umeainisha ukuzaji wa biashara hizo kwa kuhusisha na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali. Aidha  serikali imewekeza katika miundombinu ya Tehama ikiwemo mkonge wa taifa, kuimarisha biashara za mtandao ikiwemo kutuma na kupokea pesa , kuondoa tozo katika uingizaji kompyuta, kupunguza tozo za uanzishaji biashara pamoja na kuwajengea uwezo wabunifu kupitia vituo maalum ikiwemo tume ya taifa ya sayansi na teknolojia(COSTECH).

About the author

mzalendoeditor