Featured Kitaifa

TAKUKURU MKOA WA KINONDONI WASHEREKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUWAFARIJI WAZEE WAHITAJI.  

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bi. Bibie Msumi (wa kwanza kutoka kushoto) akimkabidhi zawadi Mwanzilishi wa Kituo Cha Kulea cha Tushikane Pamoja Foundation Kilichopo Manispaa ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam.

Mzee Philipo Mchopa kutoka Kituo Cha Tushikamane Pamoja Foundation akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea zawadi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni.

Wafanyakazi Wanawake wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea Kituo cha Kulea Wazee cha Tushikamane Pamoja Foundation kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji katika kituo hicho

………………………………………………………….

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni leo imeadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa kwenda kuwafariji wahitaji katika Kituo cha Kulea Wazee cha Tushikamane Pamoja Foundation kilichopo Manispaa ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika kufariji Wazee wa Kituo cha Tushikamane Pamoja Foundation, Wanawake TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni wametoa sadaka ya vitu mbalimbali ikiwemo Mchele, Unga wa Mahindi, Mafuta ya kupikia pamoja na sukari.

Akizungumza baada ya kukabidhi sadaka kwa wahitaji, Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bi. Bibie Msumi, amesema kuwa mwaka huu wameamua kusherekea siku ya wanawake duniani kwa kutoa sadaka kwa wazee kutokana wameonekana kuwa na uwitaji.

Amesema kuwa sadaka waliotoa ni sehemu ya kusherekea siku ya wanawake duniani, huku akitoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kutoa kiasi chochote kama sadaka kwa wahitaji wakiwemo watoto yatima.

“Taasisi nyengine, vikundi mbalimbali chochote kile mtakachopata pelekeni kwa watu wenye uwitaji kama tulivyokuja sisi hapa kuwapa wazee, sio lazima kiwe kikubwa wenyewe wanajua kitawasaidia na hakuna kidogo katika kutoa sadaka” amesema. Bi. Msumi.

Mchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bi. Dorothea Mrema, amesema kuwa kujumu lao ni kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na kushirikiana na jamii katika nyanja mbalimbali.

“Sisi ni wazee watarajiwa, tumekuja kusambaza upendo kwa kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali, tunaomba tuendelee kuwa pamoja katika kushirikiana” amesema Bi. Mrema.

Mwanzilishi wa Kituo cha Kulea Wazee cha Tushikamane Pamoja Foundation Bi. Rose Mwapachu, amewashukuru wanawake kutoka katika Taasisi ya TAKUKURU Mkoa Kinondoni kwa sadaka yao ambayo wanakwenda kuitumia zaidi ya miezi miwili katika mahitaji ya chakula.

“Naomba isiwe mara ya mwisho kuja kututembelea, undugu na urafiki huu uendelee kila siku pale mtakapo pata nafasi karibuni tena, Mwenyezi Mungu awabariki” amesema Bi. Mwapachu.

Hata hivyo ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto kubwa iliyopo katika kituo hicho ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi pamoja na usafiri wa kuwapeleka wazee hospitali kupata huduma ya matibabu pale wanapokuwa wagonjwa.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Kituo cha Tushikamane Pamoja Foundation, Mzee Philipo Mchopa,  amesema kuwa leo imekuwa ni siku ya baraka kwao baada ya kupata zawadi ambayo inakwenda kuwa msaada katika mahitaji ya chakula.

“Tunashukuru sana kwa kujitoa, kuwa na moyo mzuri, kwani wengine wamekuwa na tabia ya kutowajali wazee na kuwaacha bila msaada, muendelee kutujali bado tunawaitaji msitochoke, hongereni sana wanawake” amesema Mzee Mchopa.

Amesema kuwa kitendo cha kutoa sadaka ni ibada kubwa, kwani watu wanaweza wakasali kila siku kanisani na bado ikawa sawa na bure, uku akiishauri jamii ifanye ibada kwa njia ya matendo kwani ni bora zaidi.

Ameipongeza TAKUKURU kwa kuendelea kufanya kazi ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa sababu rushwa ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu na ni adui mkubwa wa  haki.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Ubungo Bi. Zainabu Masilamba, amesema kuwa kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wazee kutoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Bi. Masilamba ameeleza kuwa katika jitiada za kupunguza wazee waliotelekezwa na ndugu zao, wameendelea kutoa elimu katika vikundi mbalimbali kuhusu kuwatuza wazee.

Amefafanua kuwa unyanyasaji kwa wazee kwa kiasi fulani unatokana na mzee wenyewe kutowajibika katika kipindi cha malezi ya mtoto wake akiwa mdogo.

“Wazee wa kiume ni wengi ambao wametelekezwa na watoto wao, tunashauri wakina baba wawatuze watoto wao, kwani katwimu zinaonesha wakibaba ni wengi wanatelekeza watoto kuliko wakinamama” amesema

About the author

mzalendoeditor