Featured Kitaifa

WANAFUNZI 6 MBARONI KWA KUCHOMA PIKIPIKI YA MWALIMU

Written by mzalendoeditor

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia wanafunzi sita wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Kata ya Majengo Wilaya ya Singida kwa tuhuma za kuchoma moto pikipiki ya mwalimu yenye namba za usajili MC 653 BFS pamoja na kufyeka mahindi yaliyooteshwa katika shamba la mwalimu huyo lenye ukubwa wa ekari moja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Stella Mutabihirwa amezungumza mbele ya waandishi wa habari na kusema tukio hilo limetokea baada ya kuadhibiwa kwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne kwa kosa la kumiliki simu kinyume na taratibu za shule hiyo.

“Taratibu za shule hiyo haziruhusu mwanafunzi kuwa na simu, wakati upekuzi wa walimu unaendelea kuna mwanafunzi mmoja alitoka kwenda kuficha simu darasani, ndipo mwalimu baada ya kugundua akamuadhibu huyo mwanafunzi.

“Jioni yake wanafunzi hao wakajipanga na kwenda kuchoma pikipiki na shamba, Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio na kujiridhisha juu ya pikipiki hiyo kuchomwa na shamba kufyekwa. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa kusababisha uhaibifu,” anasema ACP Stella Mutabihirwa.

About the author

mzalendoeditor