Featured Kitaifa

ZAIDI YA MAKAMPUNI 120 TANZANIA NA NCHI JIRANI KUSHIRIKI MAONYESHO YA KIMATAIFA

Written by mzalendoeditor
………………………………………………………
Happy Lazaro,Arusha

Zaidi ya makampuni 120 kutoka Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki yatarajiwa kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya kilimo yanayojulikana Kama “TANZFOOD Expo “yatakayofanyika katika viwanja vya magereza vilivyopo mkoani Arusha kuanzia machi 11 hadi 13.

Maonesho hayo ambayo yameandaliwa na kampuni ya KILIFAIR Promotion yanalenga kukuza sekta ya kilimo ,ambapo Taasisi hiyo inaongoza katika kuandaa maonesho ya biashara ya kimataifa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo machi 1 jijini Arusha ,Mmoja wa wakurugenzi wa KILIFAIR Promotion ,Dominic Shoo amesema kuwa, ufunguzi huo utazinduliwa na Waziri wa kilimo, Hussein Bashe pamoja na Balozi wa ujerumani nchini Tanzania ,Regina Hess .
“Tunaelewa kwamba sekta ya kilimo si tu kwa ajili ya Taifa letu la Tanzania bali inalisha nchi nyingine  za kusini mwa jangwa la Sahara ,ndo  sababu tuliamua kuwekeza katika maonesho yenye viwango vya kimataifa ili tujivunie vya kutosha na kuonesha ladha ya Tanzania kama kibwagizo cha maonesho hayo.”amesema Shoo.
Naye Mkurugenzi wa KILIFAIR ,Tom Kunkler amesema kuwa,wamefurahishwa Sana kuona mwitikio wa waoneshaji kutoka ndani ya Tanzania na masoko mengine kwani maonesho hayo sio tu yataonesha bidhaa,bali itawaleta wataalamu mbalimbali wa sekta ya kilimo ili kutoa ujuzi wao kamilifu kwa makampuni yanayoshiriki na wakulima watakaofika katika maonesho hayo.
 Kunkler amesema kuwa,ndani ya siku hizo tatu za maonesho kutakuwepo na semina ili kuwaelimisha wakulima kuhusu kuongeza ubora na maendeleo katika sekta hiyo.
Amesema kuwa, wakulima hao watapata fursa ya kujifunza na kuona viwango mbalimbali katika sekta hiyo na kuweza kufikia viwango vya kimataifa katika kuuza bidhaa zao na kupata uhakika wa masoko,ambapo maonesho haya yatakuwa yanafanyika kila mwaka.
Amesema kuwa,tukio hilo la siku tatu limegawanyika katika siku za wafanyabiashara (B2B)ambapo kutakuwa na siku za watumiaji huku wageni wakitumia kujenga mtandao wa kibiashara katika mazingira rafiki ya kitaalamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa sekta ya uzalishaji kutoka EAC,Jean Havugimana  akizungumza kwa niaba ya Katibu mkuu wa EAC ,Peter Mathuki amesema kuwa,wao wakiwa kama miongoni mwa wadhamini katika maonesho hayo wamewekeza kiasi kikubwa Sana katika kuwajengea uwezo wakulima wa hapa nchini na wadau wengine wa kilimo kwa kuwapatia fursa rahisi katika sekta hiyo kupitia upatikanaji wa fedha zinazohitajika ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kilimo.

About the author

mzalendoeditor