Uncategorized

SPIKA DKT. TULIA ASIKITISHWA NA UZEMBE WA VIONGOZI KUKWAMISHA MAENDELEO MBEYA

Written by mzalendoeditor


 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesikitishwa na kitendo cha Halmashauri hiyo pamoja uongozi wa shule ya msingi Iganjo kuchelewesha ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu na matundu ya vyoo 24 ya shule hiyo licha ya yeye kufanikisha upatikanaji wa shilingi Milioni 100 za ujenzi huo.
 
Tukio hilo limetokea leo Machi 3, 2022 wakati alipofanya ziara katika kata ya Igawilo kwa lengo la kuzungumza na wananchi pamoja na kujionea maendeleo ya shule hiyo ambayo siku za karibuni aliombwa kutatua changamoto mbalimbali kwenye shule hiyo ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
 
 “Mzigo huu naitwisha halmashauri, naitwisha kwasababu fedha zinapokuja huku wao ndio watu wa kwanza kupata taarifa na ni kazi yao kuhakikisha shule hizi zinakuwa sawa. Sisi tunatafuta fedha kwa ajili ya kupunguza hizi changamoto za watoto ajabu ni kwamba kazi haifanyiki kwa kigezo eti mchakato, mchakato gani unaofanyika hapa?” amesema Dkt. Tulia
 
Pamoja na hayo, Dkt. Tulia amemuagiza Mstahiki Meya wa Jiji hilo kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo na uongozi wa shule wasimamie zoezi la ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja kwakuwa ameonesha uzoefu wa kusimamia zoezi kama hilo katika ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 hivyo kwa Imani hiyo ataweza kufanikisha kazi kwa wakati.
 
Kwa upande wake Mstahiki Meya Mhe. Dourmohamed Issa, amemuhakikishia Dkt. Tulia kwamba atatekeleza hatua hiyo ndani ya muda stahiki ili wanafunzi wa shule hiyo waweze kusoma katika mazingira safi na rafiki.
 
Naye mwananchi wa Kata ya Igawilo Aziz Ngole, kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo amemshukuru na kumpongeza Spika Dkt. Tulia kwa maendeleo aliyoyafanya katika kata hiyo pamoja na Jimbo hilo kwa ujumla na kumtaka asiache kuendelea kufuatilia matokeo ya misaada ambayo amekuwa akiitoa.

About the author

mzalendoeditor