Featured Kitaifa

RAIS WA TANZANIA SAMIA SULUHU HASSAN ATETA NA VIONGOZI WA DINI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na viongozi mbalimbali wa Dini mara baada ya Kikao chao kilichofanyika leo tarehe 02 Machi, 2022 Ikulu Jijini Dar Es salaam.

Viongozi wa Dini wakifatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,(hayupo pichani) wakati  akizungumza na viongozi mbalimbali wa Dini mara baada ya Kikao chao kilichofanyika leo tarehe 02 Machi, 2022 Ikulu Jijini Dar Es salaam.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mbalimbali wa Dini mara baada ya Kikao chao kilichofanyika leo tarehe 02 Machi, 2022 Ikulu Jijini Dar Es salaam.

PICHA NA IKULU

……………………………………………

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezungumza na viongozi wa dini mbalimbali kuhusu maendeleo ya nchi katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.


Miongoni mwa mambo waliyojadili ni elimu ambapo viongozi hao wamependekeza kuwepo kwa mjadala mpana kuhusu mfumo mpya utakaokidhi mahitaji ya sasa. Wamesema kuna umuhimu mkubwa wa elimu itayozalisha jamii ya wahitimu walioandaliwa kujiajiri badala ya kuajiriwa peke yake.


Viongozi hao wameomba serikali itafakari uwezekano wa kufuta kodi ya mapato kwenye fedha zinazopatikana kama misaada ya hiari ya wanachama na wafadhili kwa ajili ya kuendesha huduma zisizo za kibiashara zikiwemo huduma za wajane na yatima.


Pamoja na hayo, viongozi hao wamelipatia kipaumbele suala la uchafuzi wa mazingira. Viongozi wa dini wametoa wito kwa serikali kuhamasisha upandaji miti ya asili badala ya miti na mbegu kutoka nje ambazo nazo zinahatarisha usalama wa afya za wananchi.

Wakati huo huo, viongozi hao wa dini wametumia mkutano wao na Mhe. Rais Samia kuomba mamlaka husika kutumia busara ili kuangalia namna ya kumaliza kesi inayomkabili kiongozi wa CHADEMA, Freeman Mbowe  na wenzake.


Mapendekezo hayo yaliowasilishwa na Nelson Kisare, Askofu mkuu wa wa kanisa la Menonite, Tanzania kwa niaba ya viongozi hao wa dini pia yameelezea kuporomoka kwa maadili na ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu vya wizi, ujambazi, udhalilishaji, ubakaji, ukatili kwa wanawake na watoto na mauaji katika jamii, hali ambayo imeanza kutishia amani na usalama wa rai ana mali zao.


Viongozi hao wamempongeza Rais Samia kwa kuonyesha kuwa karibu na viongozi wa dini huku wakisihi kuwepo kwa vikao endelevu kati ya serikali na madhehebu ya dini kwa ajili ya tathmini na ufuatiliaji wa karibu.


Vile vile, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amepongezwa na viongozi hao wa dini kwa ujenzi wa mahusiano bora na nchi jirani na pia jumuiya ya kimataifa. 


Masuala mengine aliyopongezwa ni kujenga fursa za uongozi kwa wanawake na kuulinda Muungano.

About the author

mzalendoeditor