Featured Kitaifa

ELIMU YA MAGONJWA YA UKIMWI NA KIFUA KIKUU ITOLEWE MIGODINI

Written by mzalendoeditor

Na Englibert Kayombo – Geita.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Kifua Kikuu imetoa rai kwa Makampuni ya Migodi kuwa na mpango endelevu wa kutoa elimu ya kujingina na magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu kwa wafanyakazi.

Rai hiyo imetolewa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Hassan Toufiq mara baada ya Kamati kutembelea Mgodi wa Geita kuona utekelezaji wa afua mbalimbali za kupambana na UKIMWI na Kifua Kikuu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Kifua Kikuu imeupongeza Mgodi wa Geita (Geita Gold Mine) kwa kutoa elimu ya Masuala ya Ukimwi na Kifua Kikuu kazini.

“Hapa tumeona mnafanya vizuri katika kutoa elimu ya kujilinda dhidi ya magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu, hongereni sana na sehemu nyingine pia wafanye hivi ikiwa ni pamoja na kuwatunza watu wanaoishi na UKIMWI na Kifua Kikuu” amesema Mhe. Toufiq

Mhe. Toufiq amesema sehemu za Migodini huwa na watu wengi wanaopata maambukizi ya Kifua Kikuu kutokana na mazingira wanayofanyia kazi kuwa na vumbi jingi na kuitaka Migodi kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi ili kujiepusha na Ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameitaka Migodi kutoririsha maji taka yenye kemikali katika vyanzo vya maji ili kuwaepusha wananchi kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ugonjwa wa Saratani.

“Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kuongoza kwa ugonjwa wa Saratani, tumeamua kufanya utafiti kujua nini kinasababisha tatizo hilo kukua kwa kasi kubwa maana ukija Hospitali ya Magonjwa ya Saratani ya Ocean Road wagonjwa wengi ni wa Kanda ya Ziwa” amesema Dkt. Mollel.

About the author

mzalendoeditor