Featured Kitaifa

JUMUIYA YA MARIDHIANO MWANZA YAKUSANYA CHUPA 22 ZA DAMU

Written by mzalendoeditor
Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Mwanza, Michael Machumu (kulia) akishiriki kuchagia damu kwa hiari.
Mgeni rasmi wa maadhimisho ya Maridhiano Day, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Silas Wambura (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano mkoani humu, Sheikhe Mussa Karwanyi jana. 
Mmoja wa wanachama wa Jumuiya ya Maridhiano akichangia damu jana.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Mwanza,Musa Karwanyi,akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa madhimisho ya Maridhiano Day jijini Mwanza.
Kundi la Marastafarian wa jijini Mwanza,wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuchangia damu kwenye maadhimisho ya Maridhiano Day.Picha na Baltazar Mashaka 
**************************
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
JUMUIYA ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Mwanza,imekusanya chupa 22 za damu kwenye maadhimisha Siku ya Maridhiano (Maridhiano Day) na kuwataka wananchi na jamii kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ( Butimba ) kwa wananchi kupima afya na kuchangia damu kwa hiari. 

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyoambatana na uchangiaji damu,Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani humu,Sheikhe Mussa Karwanyi,alisema wananchi wajenge utamaduni wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hasa watoto,wajawazito na majeruhi wa ajali wenye upungufu wa damu.

“Rais Samia Suluhu Hassan, amewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya kuhakikisha afya za Watanzania zinaboreka na kuimarika,hivyo wananchi popote jijini Mwanza wamuunge mkono kwa uwekezaji na wachangie damu,”alisema.

Sheikhe Karwanyi alisema jumuiya hiyo ni daraja kati ya wananchi,viongozi wa dini na serikali katika utatuzi wa migogoro kwenye jamii na kuhimiza amani,hivyo damu ikikosekana hospitali ni mgogoro na jamii inakosa amani.

Kwa upande wake,Katibu wa Chama Cha Mabrocker’s Mkoa wa Mwanza,Japheth Alphonce,alisema wameguswa kuchangia damu kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita kuboresha sekta ya afya.

Kaimu Mganga Mkoa wa Mwanza, Dk. Silas Wambura,aliipongeza jumuiya hiyo kwa kuhamasisha jamii kuchangia damu kwenye maadhimisho hayo ya siku ya mariadhiano ili kuokoa maisha ya wananchi wenye uhitaji.

Alisema Mkoa wa Mwanza una changamoto ya damu ambapo kwa wastani zinahitajika chupa 200 hadi 300 kwa mwezi na umejiwekea malengo kila halmashauri ikusanye damu ili kutosheleza mahitaji ya wagonjwa.

“Changamoto ya damu ni kubwa na tunapata wastani wa asilimia 60 hadi 70 tu ya mahitaji halisi ya bidhaa hiyo isiyozalishwa kiwanda bali binadamu wenyewe ingawa kitaifa tunafanya vizuri baada ya kuunda timu za uhamasishaji na ukusanyaji damu,”alisema.

Dk. Wambura alisema mikakati iliyopo ni kujenga uelewa wa pamoja wa wananchi na jamii na kadiri wanavyokwenda ipo siku watatambua umuhimu wa damu na kuchangia.

Alifafanua kuwa kwa muda mrefu wanawatumia wananchi wa vyuo na sekondari kupata damu kwa matumizi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwenye hospitali mbalimbali mkoani humu.

“Wakiwa wadogo wakaelimishwa umuhimu wa kuchangia damu na wakaelewa umuhimu huo,watakapokuwa wakubwa watakuwa mabalozi wazuri na watajitokeza wenyewe bila kuhamasishwa,”alieleza Dk. Wambura.

Awali Katibu wa Jumuiya hiyo, Michael Machumu,alisema walisukumwa kuchangia damu kwenye Hospitali ya Butimba ili kunusuru maisha hasa ya wanawake wajawazito,watoto wachanga na majeruhi kutokana na hospitali nyingi kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa damu.

About the author

mzalendoeditor