Featured Kitaifa

WANANCHI KONDOA WATAKIWA KULINDA MIUNDOMBINU YA ANWANI ZA MAKAZI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka ,akiweka alama ya kuonyesha mitaa, barabara ya Iboni wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka,akimshuhudia Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dk.hamis Mkanachi akiweka zege kwenye kibao cha kuonesha mtaa tukio lililofanyika wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka,akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dk.hamis Mkanachi mara baada ya  kuweka alama za mitaa, barabara pamoja na vibao vya namba za nyumba zoezi  lililofanyika wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Barabara ya Iboni mara baada ya kuweka alama za mitaa, barabara pamoja na vibao vya namba za nyumba zoezi hilo limefanyika wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.

Madarasa yaliyobomoka katika shule ya Msingi IBONI, ambayo yalikuwa yakitumika na wanafunzi wenye ulemavu

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na watumishi pamoja Wakuu wa Shule ya Msingi na Sekonadri  wilayani Kondoa mara baada ya kuweka alama za mitaa, barabara pamoja na vibao vya namba za nyumba.

……………………………………………………

Na Bolgas Odilo-KONDOA

WANANCHI wa Wilaya ya Kondoa wametakiwa kuhakikisha wanalinda miundombinu inayowekwa na Serikali kwa kuwa jukumu la ulinzi ni la kila mmoja.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka, wakati wa ziara ya kuzindua na uwekaji wa alama za mitaa, barabara pamoja na vibao vya namba za nyumba katika wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma.

Mtaka amesema kuwa  pamoja na wilaya zote za mkoa wa Dodoma kuanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika uwekaji wa anwani za makazi lakini ipo haja ya kila mmoja kuwa mlizni wa kutunza hizo alama zinazowekwa hivyo wananchi na kila mkazi wa Kondoa analo hilo jukumu la kutunza na kulinda.

“Kuna watu wanafanya biashara ya uuzaji wa vyuma chakavu lakini wasije kuthubutu kuchukua nyara za serikali, niwaombe kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake kwa sababu ulinzi unaanza na wewe mwenyewe.

“lakini sambamba na hayo niwatake madiwani na wenyeviti wa mitaa kuweka sheria ndogondogo zitakazo saidia kulinda miundombinu hii,” amesisitiza Mtaka

Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Wakuu wa shule za Sekondari kuhakikisha wanaongeza weledi na ufanisi katika utendaji wao wa kazi ili  wanafunzi waweze kufanya vizuro katika mitihani yao ya mwisho.

Mtaka amesema kuwa  anatamani kuona Mkoa wa Dodoma unafanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne na kidato cha pili na kuongeza kuwa hii itaongeza thamani zaidi katika mkoa wa Dodoma kwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya nchi.

“Inasikitisha sana kuona shule zetu ambazo zipo Makao Makuu ya nchi tunafanya vibaya katika elimu hasa matokeo ya kidato cha nne na kidato cha pili, hivyo niwaombe mkafanye kazi kwa weledi wa hali ya juu ili tuepuke aibu hii.

“Sijaja hapa kutania na wala sina masihara katika hili, sitarajii kuona matokeo mabaya yakiendelea katika mkoa wetu ambao ndiyo makao makuu ya nchi.,” amefafanua Mtaka

About the author

mzalendoeditor