Mkuu wa mashitaka kwenye mahakama ya uhalifu wa kimataifa Karim Khan mapema leo ameeleza wasi wasi wake kutokana na uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Khan ameongeza kwamba mahakama yake huwenda ikachunguza ikiwa kumetokea uhalifu wa kivita nchini humo. Kupitia taarifa Khan amesema kwamba amekuwa akifuatilia matukio nje na ndani ya Ukraine kwa makini.
Kufuatia hatua ya Russia ya kujichukulia jimbo la Ukraine la Crimea, Machi 2014, pamoja na mapigano yaliyofuata mashariki mwa taifa hilo kati ya waasi wanaoungwa mkono na Russia na wanajeshi wa serikali ya Ukraine, taifa hilo lilikaribisha ICC kuchunguza na kufungua mashitaka dhidi ya ukatili wa binadamu na uhalifu wa kivita, uliyotekelezwa tangu Februari mwaka huo.
Decemba mwaka wa 2020, ofisi ya muongoza mashitaka ya ICC iltangaza kwamba kulikuwa na kila sababu ya kuamini kwamba uhalifu wa kivita ulitekelezwa wakati wa ghasia mashariki mwa Ukraine. Uchunguzi wa mwanzo ulikamilikia lakini ombi rasmi kwa majaji wa mahakama hiyo kuanza uchunguzi kamili bado halijatolewa.