Featured Kitaifa

SERIKALI KUKARABATI MAKAZI YA WAZEE MISUFINI TANGA,DK.CHAULA AFUNGUKA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, akikagua majengo na miundombinu ya makazi ya wazee ya Misufini, Wilaya ya Muheza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, akizungumza na wazee wanaoishi kwenye makazi ya wazee ya Muheza yaliyopo eneo la Misufini alipotembelea makazi hayo kukagua utekelezaji wa majukumu katika makazi hayo.Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Tullo Masanja, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Issa Misumari.

Wazee wanaoishi katika makazi ya Mwanzange na Misufini kwa nyakati tofauti wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, alipo zuru makazi hayo. 

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula na wazee wanaoishi katika makazi ya Misufini, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza alipotembelea makazi hayo katika ziara yake mkoani Tanga.
 
(Picha na Habari zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini MJJWM)
……………………………………………
Na MJJWM, Tanga
 
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeazimia kukarabati makazi ya wazee ya Muheza mkoani Tanga hivi karibuni ili kuimarisha mazingira ya kuishi kwa wazee wanaolelewa katika makazi hayo.
 
Akizungumza na wazee hao alipotembelea makazi hayo Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema wazee wana haki ya kupata huduma bora kwa ustawi wa afya zao.
 
Dkt. Chaula amewahakikishia wazee hao 20 wanaoishi kwenye makazi hayo kuwa muda si mrefu shughuli ya kukarabati majengo na miundombinu ya umeme, maji na barabara itaanza.
 
Ameongeza kuwa, Serikali haijawaacha wazee kwa kuhakikisha wanaishi vizuri katika makazi yote 14 yaliyopo nchini hivyo ziara yake ina lengo la kuona namna ya kuboresha makazi hayo ili yafanane na ustawi wa nchi.
 
“Tumekuja kuangalia ni namna gani  tutaboresha makazi haya yafanane na nyumba nzuri tunazopenda kuishi, kwa hiyo Serikali imetupa jukumu la kuhakikisha ustawi wenu unaimarika” amesema Dkt. Chaula.
 
Awali, Afisa mfawidhi wa makazi hayo Mwamvita Kilima amebainisha kuwa, changamoto za makazi hayo ni maji, umeme, uzio na uchakavu wa majengo.
 
Hata hivyo Mwamvita amesema, anapata ushirikiano mzuri wa Halmashauri katika kuwatunza wazee hao hususani huduma za afya.
 
“Namshukuru Mkurugenzi wa Halmshauri na timu yake, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Uviko wazee wote walipatiwa elimu na wote wamechanja ameongeza Mwamvita.
 
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Issa Misumari aliyekuwepo kwenye Ziara hiyo, aliwahakikishia wazee hao kuwa,  Halmashauri itaendelea kuwaangalia na kutoa ushirikiano kwa kuwawekea mazingira bora zaidi.
 
Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake Mzee Joseph Misigaro ameishukuru Serikali hususani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wazee.

About the author

mzalendoeditor